Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa,
akizungumza jambo mbele ya wanachama wa
Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) jijini Dodoma.
Kamishina wa Madini Mhandisi David Mulabwa aliyemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, amezindua Duka la bidhaa za Madini linalomilikiwa na Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA).
Uzindu huo umefanyika Novemba 3 katika Viwanja vya African Dream vilivyopo jijini Dodoma.
Sambamba na uzinduzi huo, Kamishna Mulabwa ametembelea mabanda mbalimbali yanayoonesha bidhaa mbalimbali zitokanazo na madini zinazotengenezwa na kuoneshwa na chama hicho.
Aidha, Kamishna Mulabwa, amekipongeza TAWOMA kwa hatua nzuri kilichofikia katika kujiletea maendelo ikiwemo kuwaelimisha wachimbaji wengine hususan wanawake.
“Ninawapongeza sana TAWOMA kwa juhudi zao wanazozifanya katika kuleta maendeleo kwenye sekta ya madini, pia nichukuwe fursa hii kuwashukuru TAWOMA maana wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wachimbaji wengine hususan wanawake”, amesema Kamishna Mulabwa.
Katika uzinduzi huo, Kamishina Mulabwa ameahidi kufanya kazi bega kwa bega na Chama hicho ili kukisaida pindi kinapohitaji msaada kutoka serikalini.
“Sisi kama Serikali tutakuwa bega kwa bega na TAWOMA na tuko tayari kuwasaidia pale mtakapo hitaji msaada kutoka Serikalini, karibuni milango iko wazi,” ameongeza Kamishna Mulabwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Chama hicho kupatiwa mikopo, Kamishna Mulabwa amesema, tayari Wizara ya Madini imeshaanza kuzielimisha taasisi za fedha ili ziweze kutoa mikopo ya vifaa na fedha kwa wachimbaji wadogo nchini ikiwemo TAWOMA ili kuwazesha kupata mikopo na waweze kuchimba kwa faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa TAWOMA aliyechaguliwa na chama hicho Desemba 3, 2020, Gilly Mtinda Raja amewashukuru wanachama wa TAWOMA kwa kumuamini na kumchagua yeye kukiongoza chama hicho ambapo ameahidi kuto waangusha na kuhakikisha chama hicho kinakua.
Pia, Raja amemshukuru Kamishna wa Madini kwa kuzindua duka hilo la kimkakati la bidhaa zitokanazo na madini ambapo, ameomba ushirikiano wa Serikali ili Chama kiweze kufanyakazi kwa pamoja na kuwaletea wanawake maendeleo.
Vile vile, amewahakikishia wanachama wa TAWOMA kwamba Serikali itahakikisha chama hicho kina wawezesha wanachama wake ili wafanyekazi zao za uongezaji thamani madini na kuyapeleka sokoni kwa tija na kwa faida.
Nae, Mwenyekiti mstaafu wa Chama hicho, Eunice Negele amesema, TAWOMA imeshaandaa mazingira mazuri ya kuhakikisha maduka ya TAWOMA yanayoshughulika na uuzaji wa bidhaa zitokanazo na madini yanafunguliwa nchi nzima.
0 comments:
Post a Comment