METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, November 19, 2020

Waziri Mkuu azindua uchepushwaji wa maji katika mradi wa JNHPP




Na Zuena Msuya, Pwani

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua njia ya mchepuko ya kupitisha maji kwenye mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kuruhusu ujenzi wa tuta kuu la kuzuia maji ya bwawa yatakayozalisha umeme.

Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 18 Novemba, 2020, katika eneo la Mradi, Rufiji mkoani Pwani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wanaohusika na Sekta ya Nishati katika nchi za Tanzania na Misri.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema kuwa, mradi huo utakaozalisha megawati 2115 ni mkubwa, wa kimkakati na aina yake  katika ukanda wa Afrika ambapo unashika nafasi ya nne kwa ukubwa, pia ni wa kwanza kwa Afrika Mashariki na Kusini.

Alieleza kuwa, Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unatekelezeka kwa wakati kwani utapelekea kuwepo kwa umeme mwingi, wa kutosha na wa gharama nafuu utakaoboresha hali ya uchumi wa nchi na wananchi.

Aliongeza kuwa, mradi huo utakapokamilika utawezesha taifa kuongeza mapato yake kwa kuongeza shughuli za kiuchumi, pia kufanya biashara ya umeme kwa nchi jirani na zenye uhitaji na pia umeme huo utatumika katika viwanda nchini.

Aliweka wazi kuwa, Serikali inaugharamia mradi huo kwa asilimia 100 na hadi sasa tayari mkandarasi ameshalipwa shilingi Trilioni 1.57  kulingana na kazi zilizofanyika, na  mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi Trilioni 6.55 hadi kukamilika kwake.

“Watanzania tujivunie kwa kuwa na mradi huu, tutembee kifua mbele kwa kuweza kutekeleza mradi huu wa JNHPP, nawahakikishia kuwa mahusiano kati yetu na makampuni yanayotekeleza mradi ni mazuri, hatuna deni lolote kwa hatua iliyofika mpaka sasa.”alisema

“Aidha, natoa wito kwa wataalam wetu wa ndani kutumia fursa hii ya kujengewa uwezo, kujifunza kila wanachokifanya watalaam kutoka nje ili waje kusaidia katika miradi mingine.”Alisisitiza

Kuhusu utekelezaji wa mradi huo, alisema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wa bwawa la kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji.

Pia, aliipongeza  Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO) kwa hatua waliyofikia katika ujenzi wa bwawa hilo na kuwataka kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa au hata kabla ya muda huo.

Vilevile aliwasisitiza wasimamizi wa mradi huo kufanya kazi zao kwa weledi, uzalendo na kuweka mbele maslahi ya taifa na kwamba wahakikishe makubaliano ya kutekeleza miradi ya kijamii kama ilivyoelekezwa katika mkataba yanatekelezwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisema kuwa, utekelezaji wa mradi huo utaenda sambasamba na utekelezaji wa miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo karibu, katika mkoa wa Pwani na Morogoro kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na wananchi.

Mhandisi Said alisema tayari mradi huo umeshatoa ajira za moja kwa moja 6,364, ambapo watanzania 5,728 wamenufaika na ajira hizo.

Alisema kuwa, mkandarasi atatekeleza miradi miwili ya kijamii ambayo ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 41 kutoka stesheni ya treni ya Fuga hadi katika eneo la mradi na ujenzi wa kiwanja cha cha kisasa cha michezo kinachotarajiwa kujengwa mkoani Dodoma.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuridhia na kutoa fedha za kutekeleza ujenzi wa mradi huo bila vikwazo vyovyote hadi hapo ulipofikia huku shughuli za ujenzi zikiendelea kwa kasi inayoridhisha.

Hata hivyo aliwashauri wasimamizi na wakandarasi wanaotekeleza  mradi huo kufanya kazi kwa bidii na maarifa, huku wakijua kuwa mradi huo unatekelezwa  kwa manufaa ya watanzania na taifa kwa ujumla.

Aliwahamasisha wawekezaji kutumia fursa hiyo kuja kuwekeza zaidi nchini kwa kuwa kutakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na gharama nafuu kuweza kuendesha shughuli za kiuchumi na pia Tanzania ina sera nzuri na bora za kuwavutia wawekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com