Baadhi ya viongozi wa dini na chifu wa Kabila la Wabende Mkoani Katavi wamekemea vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu wenye kusudi la kukwamisha mipango ya maendeleo inayofanywa na Serikali kwa nia ya kuihujumu na Serikali na kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania hususan vijana.
Onyo hilo limetolewa sambamba na Uzinduzi wa Kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliofanyika Mkoani Katavi ukibebwa na Kaulimbiu Twende Pamoja, Ukatili Tanzania sasa Basi.
Viongozi hao wamesema kutokomeza ukatili nchini kunaenda sambamba na kukemea kauli za baadhi ya watu wenye nia ovu wanaowachochea vijana kuichukia Serikali yao kwa manufaa yao binafsi.
Kwa nyakati tofauti wamesema uchaguzi Mkuu umekwisha na viongozi wamepatikana kwa haki na kama ilivyo katika vitabu vya dini hakuna sababu ya kuendelea kuchochea chuki kwa lengo la kusababisha machafuko na badala yake ni muhimu kuheshimu mamlaka.
“Hivi karibuni tulikuwa na uchaguzi Mkuu ambapo viongozi wetu wamepatikana kwa haki,wameapishwa na wanaendelea kutuongoza katika kuelekea uchumi wa juu”
“Asitokee mtu anayekusudia kuhujumu juhudi za Serikali hii ya awamu ya tano ambayo jitihada zake zimedhihirika kwa mambo mengi katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John Magufuli” alifafanua Askofu Julius Mussa wa Makanisa ya Free Pentecost Church of Tanzania.
Viongozi hao wamesema kwa siku za hivi karibuni kuna baadhi ya watu wanaotoa kauli zenye viashiria vya kuvunja amani ya nchi na hivyo kukwamisha maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.
Viongozi hao wamesema Rais John Magufuli na timu yake ya uongozi tayari imejipambanua kwa kuongoza Watanzania kujiletea maendeleo yao na mambo mengi yaliyofanyika katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya awali ya tano yanaonekana bayana hivyo hakuna sababu za kutumia propaganda chafu za kuhatarisha amani iliyopo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo, Katibu Mkuu,Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Dkt. John Jingu amewataka Watanzania katika ngazi zote kuungana na kupinga vitendo vinavyolenga kuhujumu mipango ya Serikali.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Dkt. Jingu amesimikwa kuwa mmoja wa machifu wa Kabila Wabende kwa kukabidhiwa zana za kimila ikiwa ni sehemu ya kutambua kazi anayoifanya hasa za kupambana na vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto.
Akizungumza wakati akimsimika uongozi, Chifu Kapalampya Lumbwe wa Kabila hilo amesema amemvalisha vazi maalum lenye rangi nyekundu na nyeupe kuashiria uimara na amani pamoja na kupewa silaha za jadi za kabila la Wabende.
0 comments:
Post a Comment