Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachewene akizungumza katika Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni akimuwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho haya yamefanyika Jijini Dodoma na yameenda sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi wa insha kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Hifadhi ya Bioanuai kwa wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachewene akikabidhi zawadi kwa mshindi wa pili wa insha kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Hifadhi ya Bioanuai kundi la Shule za Msingi Bi. Rachel William Mbonea kutoka Shule ya Msingi Barney iliyopo Dar es Salaam.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachewene akiwa katika picha ya pamoja
na washindi wa Insha kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Hifadhi ya Bioanuai.
Washindi hao ni kutoka Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu.
Hafla hii imefanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Wengine katika
picha ni Balozi Joseph Sokoine Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi.
Vumilia Nyamoga Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Bw. Faraja Ngeregeza
Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira – Ofisi ya Makamu wa Rais.
Tanzania imepunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa tabaka la ozoni azma ikiwa ni kuondosha matumizi ya kemikali hizi kufikia mwaka 2030.
Haya yamesemwa hii leo Jijini Dodoma
na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
katika kuadhimishia Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kupitia
Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.
George Simbachawene.
Alisema, katika jitihada za kuhifadhi Tabaka
la Ozoni, mwaka 1996, Serikali ya Tanzania iliandaa na kutekeleza Programu ya
Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa tabaka la ozoni ili
kuhakikisha kwamba hakuna sekta ya uchumi au jamii inaathirika kutokana na
matakwa ya Itifaki ya Montreal. Aidha, programu hii ilianzisha utaratibu wa
kusimamia na kudhibiti uingizaji wa
kemikali na bidhaa zenye kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka nje ya
nchi.
Kwa upande mwingine Mheshimiwa Makamu wa Rais
aliikumbusha jamii wajibu wa kuendelea kulinda tabaka la ozoni kwa kuepuka kuingiza nchini kemikali na vifaa vinavyotumika kumong'onyoa tabaka
la ozoni kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba) bali
kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni.
“Natoa
rai kwa jamii kununua bidhaa zilizowekwa nembo ya “Ozone friendly” yaani
‘sahibu wa Ozoni’ au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na
kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, kuepuka kutupa ovyo majokofu ya
zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni”
Alisisitiza Makamu wa Rais.
Maadhimisho
ya mwaka huu yalienda sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi wa insha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na
hifadhi ya bioanuai kwa ngazi za Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu
ya Juu kwa lengo la kukuza na kupima uelewa,
kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi na vijana kuhusu mabadiliko ya tabianchi na
hifadhi ya bioanuai.
Pia
alitoa wito kwa washirika wa maendeleo kuunga mkono jitihada za kutunza
mazingira katika: kuhifadhi tabaka la ozoni; kukabiliana na kuhimili mabadiliko
ya tabianchi; kuhifadhi bioanuai na usafi wa mazingira. Pia, kuhusisha vijana
wadogo na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za mazingira ili kuwa na kizazi
chenye uelewa na kinachothamini hifadhi ya mazingira.
Awali, Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi
Joseph Sokoine alisema juhudi za kulinda Tabaka la Ozoni zinaendelea kupata
mafanikio duniani na kusisitiza kuwa huenda litarejea katika hali yake ya awali
takribani miaka 30 mpaka 50 ijayo endapo hapatakuwa na kemikali haribifu
zitakazoingia tena angani. “Juhudi zozote za kupunguza matumizi ya kemikali
hizo zitaleta matokeo ya manufaa kwenye kurejesha tabaka la Ozoni katika hali
ya kawaida. Juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha
madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na shughuli zetu tunazofanya”
alisisitiza Balozi Sokoine.
Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya ardhi likiwa na kazi ya kuchuja kiwango kikubwa cha mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Miaka 35 ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa manufaa ya afya ya binadamu na mazingira” (Ozone for Life - 35 years of Ozone Layer Protection). Kaulimbiu hii inatukumbusha umuhimu wa kulinda na kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa Tabaka hili.
0 comments:
Post a Comment