METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, September 4, 2020

TATIZO LA MAJI SIMANJIRO KUWA HISTORIA-MAJALIWA


 Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka katika mkutano wa kampeni za CCM  uliofanyika Orkesumet wilayani Simanjiro, Septemba 4, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Wananchi  wa Orkesumet wakimpungia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni  za CCM katika jimbo la Simanjiro, Septemba 4, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na mgombea Ubunge jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka wakishuhudia  wakati  Neema Nakembetwe aliposoma hadharani Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025 kifungu kinachozungumzia ujenzi wa barabara  ya Kongwa mkoani Dodoma hadi KIA kupitia wilayani  Simanjiro kwa kiwango cha lami. Mheshimia Majaliwa alimwita Neema asome kifungu hicho wakati aliposimama katika kijiji cha Lendanai  baada ya kukuta wananchi wengi wamejipanga barabarani wakiwa na kiu ya kumsikiliiza. Alikuwa akitoka Orkesumet wilayani Simaniro ambako alihutubia mkutano wa kampeni, Septemba 4, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Simanjiro kuwa historia baada ya Serikali kujenga mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet wenye thamani ya sh bilioni 40.

 

“Mradi huu umefikia asilimia 89 za utekelezaji na unatarajiwa kuanza kufanya kazi mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba 2020 au mapema Oktoba 2020. Pia Serikali imetekeleza miradi mingine ya maji ikiwemo ya uchimbaji ya mabwawa ya kunyweshea mifugo ambayo tayari inatoa huduma kwa wananchi.”

 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 4, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Orkesumet wilayani Simanjiro mkoani Manyara wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na wagombea udiwani.

 

Mheshimiwa Majaliwa ametaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo wa kutoa maji kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet wilayani Simanjio kuwa ni Irkujit ambapo tayari miundombinu ya maji imeshafika kijijini. “Vijiji vingine ni Irkirungrung, Endonyongijape, Narosoito na Lorimorijoi.”

 

Amesema miradi mingine inayotekelezwa katika wilaya hiyo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu vya maji 18 katika maeneo ya Kitwai, Msitu waTembo, Mirerani, Londrekes, Loibosoit, Kityangare Namalulu, Terrat, Olbili, Nadonjukin na Okutu. Ukarabati wa visima 13 umefanyika kikamilifu hatimaye vituo vya kuchotea maji vimefikia 95.

 

“Ujenzi wa bwawa la Narakauo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na wananchi wa vijiji vya karibu yake unaendelea kupitia Wizara ya Mifugo kwa gharama ya sh.  413,865,700 sawa na asilimia 36.”

 

Waziri Mkuu amesema mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji wa ukanda wote wa Simanjiro ya juu. Pia Serikali imetumia sh. 412,724,300 kutekeleza mradi wa maji kutoka Nomokon hadi Narakauo ambao pia utasaidia kupunguza uhaba wa maji kwa wafugaji wa Kata nzima ya Loibosiret.

 

 

Amesema licha ya utekelezaji wa miradi ya maji pia, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili kuboresha barabara za mjini katika Halmashauri ya wilaya hiyo na zile za makao makuu ya wilaya (Orkesumet) ambazo zinaendelea kuwekewa lami. “WanaSimanjiro endeleeni kukiamini Chama chenu Cha Mapinduzi kwa kuchagua wagombea wote wa CCM ili mpate maendeleo zaidi.”

 

Akizungumzia kuhusu nishati ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 56 vya wilaya ya Simanjiro vijiji 38 tayari vimepata umeme na vijiji 18 visivyokuwa na umeme vitapatiwa nishati hiyo, hivyo amewataka wananchi hao waendelee kuwa na subira na kuiamini Serikali yao.

 

Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Simanjiro. Gharama za kuunganishiwa umeme huo zimepungua kutoka sh 177,000 hadi sh. 27,000.

 

Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali.

 

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao wamchague Rais Dkt John Pombe Magufuli ili aendeleze kazi ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao ambayo tayari ameshaianza. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com