METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 21, 2020

MAJALIWA: KODI NYINGI SEKTA YA UVUVI ZIMEPUNGUZWA

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya Bukima, katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika viwanja vya Bukima, wilayani Musoma Vijijin Septemba 20, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na mgombea Ubunge wa Jimbo la Musoma Vijijini,Profesa  Sospeter Muhongo,  katika mkutano wa kampeni uliyofanyika kwenye viwanja vya Bukima, wilayani Musoma Vijijini Septemba 20, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Ilani ya chama hicho ya mwaka 2015 -2020 ilielekeza upunguzaji wa kodi kwenye sekta ya uvuvi, na agizo hilo limetekelezwa.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Bukima, wilayani Musoma, mkoani Mara katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Majita.

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo na madiwani wengine wa wilaya hiyo. Mgombea udiwani wa kata ya Bukima, Bw. Januari Simla alipita bila kupingwa. 

 

"Katika kutekeleza Ilani ya CCM, tumepunguza kodi kwenye malighafi na zana za uvuvi, kwenye injini za uvuvi, nyuzi za kushonea nyavu za kuvulia samaki, vifungashio na kwenye ada za leseni za kuvulia samaki," amesema.

 

Akielezea mambo mengine yaliyofanyika kwenye sekta hiyo, amesema kazi kubwa iliyofanyika ni kuwatambua wavuvi na kuwaweka kwenye vikundi kazi ambayo alisema imesaidia kuongeza vikundi hivyo kutoka 37 hadi kufikia 113.

 

"Ni kwa nini tuliamua kuwaweka kwenye vikundi, ni kwa sababu inakuwa rahisi kuwafikia, kuwaelimisha na kuwahudumia. Hii imefanikisha idadi ya samaki wanaovuliwa iongozeke kutoka samaki 415,000 hadi kufikia zaidi ya 800,000."

 

Amesema kiwango cha uvuaji samaki kimeongezeka kutoka tani 300 na kufikia tani 448, 467. "Kikubwa ninachowaomba ni kwamba, tumieni vyombo vya kisasa kuvua samaki ili kutunza mazalio yao."

 

Akiwa njiani kuelekea Musoma Mjini, Mheshimiwa Majaliwa alisimamishwa na wakazi wa kata za Kusenyi, aliwasalimia wakazi wa kata za Mugango na Mkirira, ambako pia aliwaombea kura wagombea wa urais, ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com