Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dodoma leo Tarehe 18 Agosti 2020.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Mahitaji ya chakula kwa mwaka 2020/2021 ni kiasi cha tani 14,347,955, ikilinganishwa na tani 13,842,536 kwa mwaka 2019/2020 ambapo tani 9,131,803 ni za mazao ya nafaka na tani 5,216,152 ni mazao yasiyo nafaka.
Kutokana na mahitaji haya yakilinganishwa na uzalishaji, Tanzania inatarajiwa kuwa na ziada ya tani 3,394,434 za chakula, ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2,072,413 ni za mazao yasiyo nafaka hivyo Uzalishaji huu umeongezeka kwa kiasi cha tani 1,334,079 sawa na asilimia 7.5.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo Tarehe 18 Agosti 2020 wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dodoma na kuongeza kuwa hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo wa 2015/2016 hadi 2019/2020. Katika kipindi hicho, nchi imekuwa na kiwango cha utoshelevu kati ya asilimia 120 hadi 125 na imekuwa ikizalisha ziada kati ya tani 2,582,717 hadi 3,394,434.
Amesema katika msimu wa 2019/2020, nchi inatarajiwa kuwa na uzalishaji wa ziada ikilinganishwa na mahitaji. Mafanikio hayo yanatokana na hali ya hewa nzuri, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali pamoja na Wadau wengine wa masuala ya kilimo.
Hasunga amesema kuwa Uzalishaji wa mazao ya nafaka unatarajiwa kufikia tani 10,453,823 sawa na ongezeko la tani 1,445,914 sawa na asilimia 13.8 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 9,007,909 kwa msimu wa 2018/2019. Aidha, kwa mazao yasiyo nafaka uzalishaji unatarajiwa kufikia tani 7,288,565 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 7,400,400 kwa msimu wa 2018/2019.
Uzalishaji wa mahindi unatarajiwa kufikia kiasi cha tani 6,388,446 ikilinganishwa na tani 5,817,508 za uzalishaji wa msimu wa 2018/2019. Uzalishaji wa mchele unatarajiwa kufikia kiasi cha tani 2,942,895 ikilinganishwa na tani 2,009,174 kwa msimu wa 2018/2019.
Amesema kuwa, uzalishaji wa mahindi umeongezeka kwa tani 570,938 na mchele kwa tani 933,721 sawa na asilimia 8.9 na 31.7 mtawalia.
Waziri Hasunga amesema kuwa hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo wa 2015/2016 hadi 2019/2020.
Katika kipindi hicho, nchi imekuwa na kiwango cha utoshelevu kati ya asilimia 120 hadi 125 na imekuwa ikizalisha ziada kati ya tani 2,582,717 hadi 3,394,434. Katika msimu wa 2019/2020, nchi inatarajiwa kuwa na uzalishaji wa ziada ikilinganishwa na mahitaji. Mafanikio hayo yanatokana na hali ya hewa nzuri, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali pamoja na Wadau wengine wa masuala ya kilimo.
Amesema kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwezi Juni 2020 ilifanya Tathimini ya Hali ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula kwa msimu wa 2019/2020 na Upatikanaji wa Chakula kwa mwaka 2020/2021 katika mikoa yote 26 na kuhusisha halmashauri 184 za Tanzania Bara kwa lengo kubaini uzalishaji na mahitaji.
Matokeo ya tathmini yanaonesha kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini kwa Msimu wa 2019/2020 na Upatikanaji wa Chakula kwa Mwaka 2020/2021 inatarajiwa kufikia kiasi cha tani 17,742,338 kwa mlinganisho wa nafaka (Grain Equivalent) ikilinganishwa na tani 16,408,309 kwa msimu wa 2018/2019.
Hasunga amesema kuwa tathmini imebainisha pia kuwa kwa msimu wa 2019/2020 mahindi yatachangia asilimia 36, mchele asilimia 16.6, muhogo asilimia 14, mikunde asilimia 10.5, viazi asilimia 9.2, mtama asilimia 5.9 na ngano asilimia 0.4.
Aidha, Kwa kuzingatia Kigezo cha Upimaji wa Kiwango cha Utoshelevu (Self Sufficiency Ratio – SSR), matokeo yanaonesha kuwa kwa mwaka wa chakula 2020/2021, nchi inatarajiwa kuwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 124. Kiwango hiki kimeongezeka ikilinganishwa na msimu wa 2018/2019 katika kipindi kama hiki ambapo kiwango cha utoshelevu kilikuwa asilimia 119.
Waziri Hasunga amebainisha kuwa pamoja na uzalishaji mzuri katika kiwango cha ziada kuna baadhi ya mikoa na halmashauri ambazo zimeonesha kuwa na maeneo yenye Dalili za Kuwa na Upungufu wa Chakula Nchini.
Tathmini imeonesha mikoa 7 ina maeneo yenye dalili zitakazosababisha kuwa na upungufu wa chakula katika Halmashauri 12 ambapo Halmashauri 10 zinatoka katika mikoa yenye kiwango cha Utoshelevu, na Halmashauri 2 ni katika mikoa yenye viwango vya Ziada.
Mkoa wa Lindi [Halmashauri za Kilwa, Lindi DC, Liwale, na Ruangwa], Mkoa wa Singida [ Halmashauri za Ikungi, Itigi na Manyoni]; Mkoa wa Manyara halmashauri ya Simanjiro; Mkoa wa Simiyu halmashauri ya Meatu; Mkoa wa Mara halmashauri ya Musoma DC na Mkoa wa Rukwa halmashauri ya Sumbawanga DC.
Hali ya chakula kimkoa inatarajiwa kuwa ya kiwango cha: Ziada kati ya asilimia 126 na 237 katika mikoa 11 ambayo ni Geita, Morogoro, Kagera, Iringa, Kigoma, Njombe, Mbeya, Katavi, Songwe, Rukwa na Ruvuma; Utoshelevu kati ya asilimia 104 na 119 kwenye mikoa 14 ya Arusha, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Tabora, Mtwara, Dodoma, Lindi, Singida, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Manyara na Uhaba kwa asilimia 3 katika mkoa wa Dar es salaam.
Serikali imeendelea kuhimiza na kuelekeza wakulima kuzalisha kwa tija ili kuongeza uzalishaji. Ili kuongeza Tija, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usambazaji na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati hususani mbolea, mbegu bora, viuatilifu na zana bora za kilimo.
Katika msimu wa uzalishaji wa mazao ya chakula wa 2019/2020, wastani wa tija ya zao la mahindi kitaifa, imeongezeka kutoka tani 1.5 kwa hekta kwa msimu wa 2018/2019 hadi tani 1.6 kwa hekta.
Aidha, tija ya zao la mahindi kwa hekta katika mikoa ya nyanda za juu kusini imeendelea kuimarika ambapo katika mkoa wa Ruvuma umeongoza kwa tija ya tani 2.7, Mbeya (tani 2.6), Songwe (tani 2.5), Rukwa (tani 2.2) na Katavi (tani 2.1).
Kwa upande mpunga wastani wa tija kitaifa umeogezeka kutoka tani 3.0 kwa hekta katika msimu wa 2018/2019 hadi tani 3.4 kwa hekta msimu wa 2019/2020.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment