METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, August 19, 2020

NAIBU WAZIRI MABULA AISHUKIA HALMASHAURI YA USHETU KUSHINDWA KUTOA HATI KWA MIAKA MINNE


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga Ezekiel Kitlya alipowasili  ofisi ya Halmashauri ya Ushetu akiwa katika ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Shinyanga jana.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Michael Matomora akisoma taarifa ya ardhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi katika mkoa wa Shinyanga jana.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa sekta ya  ardhi katika halmashauri ya Msalala akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Shinyanga jana. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga Ezekiel Kitlya na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala Simon Berege.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameshangazwa na halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga kushindwa kutoa Hati ya Ardhi hata moja kwa wananchi katika kipindi cha miaka minne.

Dkt Mabula alishangazwa na hali hiyo akiwa katika ziara yake ya kikazi jana katika halmashauri ya Ushetu kufuatia kuelezwa na Mkurugenzi wa Halamshauri hiyo Michael Matomora kuwa halmashauri yake haikuweza kutoa hati katika kipindi cha miaka minne kutokana na changamoto malimbali ikiwemo upungufu wa watumishi, vifaa vya upimaji na muitikio mdogo wa umilikishaji ardhi.

Alisema, haiwezekana halmashauri ya Ushetu aliyoieleza kuwa bado ni mpya kushindwa kuandaa hati katika kipindi cha miaka minne na kumuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Ofisi ya Ardhi mkoa wa Shinyanga Ezekiel Kitlya kupeleka mtaalamu wa ofisi yake kusaidia ukamilishaji baadhi ya hati za ardhi zilizoandaliwa kwenye halmashauri.

Taarifa ya ardhi ya halmashauri ya Ushetu iliyotokana na mgawanyo wa iliyokuwa halmashauri ya wilaya ya Kahama ambayo ilihamia rasmi makao yake makuu eneo la Nyamilangano mwaka 2016 imeeleza kuwa, halmashauri hiyo ilifanikiwa kuandaa hati 335 lakini ilishindwa kuzitoa kwa wananchi jambo lililomfanya Naibu Waziri Dkt Mabula kuagiza hati hizo kukamilishwa ndani ya mwezi mmoja na kutolewa kwa wahusika.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi, kama kuna shida yoyoye ya kitaalamu kuhusiana na uandaaji hati za ardhi katika halmashauri ya Ushetu basi ofisi ya ardhi mkoa wa Shinyanga ipo aliyoieleza kuwa inaweza kusaidia kutoa msaada kwa halmashauri hiyo kurahisisha na kuongeza kasi ya utoaji hati.

‘’Mkurugenzi sasa mnakusanya nini katika kodi ya pango la ardhi badilisheni taratibu watu wamilikishwe na kupatiwa hati, halmashauri yenu bado ni mpya inahitaji mpango kabambe ili watu wasijenge hovyo’’ alisema Dkt Mabula.

Aidha, Dkt Mabula alitaka elimu itolewe kwa viongozi wa vijiji vinavyokuwa kwa kasi ili kuweza kuwanadaa wananchi wake kupanga vizuri maeneo yao kwa lengo la kuepuka ujenzi holela ili kuepuka zoezi la urasimishaji alilolielezea kuwa sio la kudumu na kusisitiza kwamba iwapo viongozi wa halmashauri watashindwa kupanga vizuri miji yao basi wategemee kuwa na miji ya hovyo na migogoro ya ardhi .

Naibu Waziri wa Ardhi alitembelea pia halmashauri ya Msalala ambapo aliwaeleza watendaji wa sekta ya ardhi kuwa halmashauri yao inatakiwa kuongeza kasi ya utoaji hati za ardhi na kuagiza kila mwezi halmashauri hiyo kuandaa hati 600.

Amezihimiza halmashauri nchini kuhakikisha maeneo yote yanayomilikiwa na taasisi za umma kupimwa na kutolewa hati kwa lengo la kuziwezesha kuwa na miliki salama na wakati huo kuepuka migogoro ya ardhi baina ya taasisi hizo na wananchi.

Naibu Waziri Mabula alimaliza ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Shinyanga ambapo mbali na mambo mengine alikagua tendaji kazi wa sekta ya ardhi na kukutana na watumishi wa sekta ya ardhi kwenye Halmashairi ya Manispaa Shinyanga pamoja na zile za Kahama, Ushetu na Msalala.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com