Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Lamadi wilayani Busega mara baada ya kukamilika kwa zoaezi la wananchi kupiga kura za siri kubaini watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani humo, ambalo limefanyika katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji cha Lamadi Februari 14,2019.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Wananchi wa Kata ya Lamadi
Wilayani Busega mkoani Simiyu wamepiga kura za siri kwa lengo la kubaini
watuhumiwa wa mauaji ya watoto yaliyotokea hivi karibuni wilayani humo.
Wakizungumza katika zoezi
hilo lililofanyika Februari 14, 2019 katika Kitongoji cha Kisesa Kijiji
cha Lamadi wananchi hao wamesema kuwa wamelipokea vizuri zoezi hilo na
kubainisha kuwa kura hizo zitasaidia Vyombo vya Dola katika kufanya uchunguzi
na kuwabaini wauaji wa watoto wilayani humo.
“Zoezi hili nimelipokea
vizuri na nina imani litatusaidia kuwapata wauaji wa watoto wetu na naishukuru
Serikali kuona haja ya kuwashirikisha wananchi maana mauaji haya ya watoto
yametusikitisha sana wakazi wa Lamadi” alisema Modesta Andrea mkazi wa Lamadi
“ Tukio hili la kupiga kura
za siri mimi naona ni zuri kwa sababu naamini kuna baadhi ya wananchi wanaweza
wakawa wanafahamu watu waliofanya mauaji ya watoto na kama ikitokea kuna watu
wakaandikwa labda kwa sababu ya fitina tunaamini vyombo vyetu vya dola vitachuja
na kuchunguza na mwishowe wauaji watabainika tu; tunaomba wakibainika sheria
ifuate mkondo wake” alisema Elisha Daniel mkazi wa Lamadi.
Akizungumza na wananchi wa
Lamadi mara baada ya zoezi hilo kukamilika, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony
Mtaka amesema kufanyika kwa zoezi hilo hatua ya kwanza ya uchunguzi wa mauaji
ya watoto wilayani humo, huku akiwahakikishia wananchi kuwa kura walizopiga
zitahesabiwa kwa haki na vyombo vya dola mkoani humo.
“Kupiga kura za siri si
kwamba tumeshindwa kufanya upelelezi, hii ni hatua ya kwanza ya sisi kufanya
uchunguzi wetu, kura hizi zitahesabiwa na vyombo vya dola mkoani Simiyu ambavyo
ni Usalama wa Taifa, Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Jeshi la Wananchi JWTZ (Mkoa
wa Simiyu), Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Polisi na TAKUKURU” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amesema
Serikali mkoani humo itaendelea kutimiza wajibu wake wa kwanza wa kulinda watu
wake na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani ili waweze kufanya vema
shughuli za maendeleo.
Sambamba na hilo Mtaka amesema
Serikali itahakikisha inayafanyia kazi masuala mbalimbali yaliyosemwa na
wananchi katika mkutano huo, ikiwa ni pamoja na malalamiko dhidi ya utendaji wa
baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali na kubainisha kuwa
hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika kwenda kinyume
katika kuwatumikia wananchi.
“Niwahakikishie kuwa
Serikali itayafanyia kazi yote yaliyosemwa na wananchi katika Mkutano wa
hadhara uliofanyika hapa Lamadi, kama kuna wakubadilishwa watabadilishwa, wa
kuwajibishwa watawajibishwa, wakuhamishwa watahamishwa naomba mniamini”
alisisitiza Mtaka.
Kwa upande wake Mbunge wa
Busega, Dkt. Raphael Chegeni ametoa pole kwa wazazi wote waliopoteza watoto wao
katika mauaji ya watoto na kuahidi kutoa rambirambi shilingi 500,000/= kwa kila
familia iliyokutwa na msiba huku akilaani vikali vitendo vya mauaji ya kinyama
ambayo yamekatisha ndoto za watoto hao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Busega, Mhe. Tano Mwera amewashukuru wananchi wa Lamadi kwa namna
walivyojitokeza katika zoezi la kupiga kura za siri na kwa namna walivyolifanya
kwa amani na utulivu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment