Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (kushoto) akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo mkoani Dodoma.
Mradi wa ujenzi wa makazi ya makao ya watoto katika makao ya nchi mkoani Dodoma unaelezwa kuwa kati ya miradi ya mfano Afrika unaolenga kusaidia kutatua changamoto ya watoto wanaofanya kazi na kuishi mtaani nchini.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo uliofanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika eneo la unapojengwa mradi huo kikombo mkoani Dodoma.
Dkt. Jingu amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya makao yenye ubora kwa ajili ya kuwapokea watoto walio katika mazingira magumu wakiwemo wale wanaoishi na kufanya kazi mitaani hivyo Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Abbott Tanzania imekuja na utatuzi utakaosaidia kumaliza changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ina dhamana ya kusimamia usajili na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwemo ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na Mashirika hayo katika kuleta mabadiliko chanja kwa jamii.
“Ninyi kama Shirika mngeweza kusema na kuonesha kwa Serikali kuwa kuna changamoto ya makao kwa watoto waishio katika mazingira magumu ila imeamua kutafuta ufumbuzi wake kwa kushirikiana pamoja nasi”alisema
Aidha Dkt. Jingu ameeleza kuwa mradi huo mpaka kukamilika kwake utarajiwa kutumia kiasi cha Shillingi za Kitanzania Billioni13 ikijumuisha ujenzi wa majengo na uwekaji wa samani na vifaa mbalimbali katika mindombinu hiyo.
“Katika hili niseme tumejifunza thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi na hapa nimeona thamani ya fedha inaendana na mradi mpaka hatua hii ilipofikia” alisisitiza
Dkt. Jingu ameilipongeza Shirika la Abbott Tanzania kwa kuwa mfano mzuri wa ushirikiano kati ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Naftali Ng’ondi amesema kuwa mradi huo ni wa kipekee ndani ya nchi na nje kwani umebuniwa na kusanifu na wataalam wa ndani kwa kushirikiana na Maafisa Ustawi wa jamii katika kuweka miundo mbinu inayohitajika kwa mazingira ya nchi yetu.
“Huu ni maradi wa mfano sio tu kwa Tanzania bali kwa Afrika kwa ujumla pale linapokuja huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu” alisema
Naye Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Vickness Mayao amelipongeza Shirika la Abbott Tanzania kwa kuwa na uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi yai ukiwemo huo wa ujenzi wa Makao ya Taifa ya Watoto.
“Lengo la Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi pamoja na pale ambapo Serikali haijafika Mashirika hayo yaweze kufanya kwa niaba ya Serikali”alisema
Awali akieleza ushiriki wa Shirika la Abbott Tanzania katika maradi huo, Mkurugenzi wa Shirika hilo Natalia Loboure ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kukubali kushirikiana Shirika lake kutekeleza mradi huo ambao utaacha alama katika mstakabali wa malezi na makuzi kwa watoto waishio katika mazingira magumu nchini.
Mradi wa ujenzi wa Makao ya Taifa ya Watoto mkoani Dodoma unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Oktoba na utakuwa na uwezo wa kuchukua watoto takribani ya 250 kwa wakati mmoja na utagharimu kiasi cha Shillingi Billioni 13 mapaka kukamilika kwake.
0 comments:
Post a Comment