WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaohitimu masomo nchini wasikae majumbani na badala yake watumie elimu yao kubuni namna ya kujiajiri.
“Lazima tubadilike ili wahitimu wasisubiri kazi za masomo. Ukimaliza masomo, tumia ujuzi wako kuona unaweza vipi kujiajiri,” alisema.
Ametoa wito huo jana jioni (Jumatatu, Agosti 17, 2020) wakati akizungumza na wahitimu wa Seneti ya Dar es Salaam kwenye mahafali ya vyuo na vyuo vikuu vya jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Karimjee, jijini humo.
“Tunajaribu kuondoa dhana ya ajira ni ile kazi ya kushika kalamu na kukaa ofisini na kulipwa mshahara mwisho wa mwezi. Sasa kama wasomi wote tukitaraji kuajiriwa, hatutaweza. Lazima tukubali kuwa ajira ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato chake,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imefanya kazi ya kuboresha mazingira ya utoaji wa taaluma kwa kujenga na kukarabati miundombinu katika baadhi ya vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu nchini.
“Ili kuondoa adha ya malazi kwa wanafunzi kwa vyuo na taasisi za elimu ya juu zilizopo Dar es Salaam, Serikali imetoa nyumba za Serikali zilizoko Kigamboni na Kijichi, jijini Dar es Salaam.”
Akizungumzia kuhusu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Waziri Mkuu alisema ujenzi wa maktaba ya kisasa inayochukua wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja uligharimu sh. bilioni 93. “Ujenzi wa mabweni 20 ya Dkt. John Pombe Magufuli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 na ukarabati wa hall 2 na 5, yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 788 uligharimu shilingi bilioni 15.48,” alisema.
Kuhusu Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE), Waziri Mkuu alisema Serikali ilitumia sh. bilioni 1.5 kujenga miundombinu ya kufundishia na ofisi za wahadhiri Katika chou hicho na pia ilitumia sh. bilioni 4.9 kufanya ukarabati mkubwa wa majengo ya Hall 2 na Hall 5 chuoni hapo.
“Kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) tulitumia shilingi bilioni 11.5 kwa ajili ya ujenzi wa maabara yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,400 kwa wakati mmoja; ujenzi wa Kafeteria ya wanafunzi pamoja na kutengeneza shamba darasa kwa shilingi milioni 700; ukarabati wa karakana ya uhandisi kwa shilingi milioni 750 na ununuzi wa matrekta 10 aina ya URSUS pamoja na majembe nane na harrow mbili kwa thamani ya shilingi milioni 587.5 ili kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa vitendo.”
Akielezea uboreshaji uliofanywa kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 716 uligharimu sh. bilioni 3.44 ilhali Chuo Kikuu cha Dododma (UDOM) kilinunuliwa vifaa vya maabara vya thamani ya sh. bilioni 3.0.
“Kwa upande wa Chuo cha Ardhi (ARU), tumeanza na awamu ya kwanza ya ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 312 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.61, Na kwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), tumejenga jengo la mihadhara lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200 kwa gharama ya shilingi bilioni 8.8. Pia tumejenga maabara kwa gharama ya shilingi bilioni 2.1,” alisema.
Kuhusu Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Waziri Mkuu alisema ujenzi wa hosteli zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,024 uligharimu sh. bilioni 6.5 huku ujenzi wa jengo la mihadhara lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 900 ulitumia sh. bilioni 3 katika kampasi ya Mzumbe-Mbeya.
Na kwa upande wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Waziri Mkuu alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa maktaba ya kisasa yenye uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 2,500 umekamilika kwa gharama sh. bilioni 5.523.
“Kwenye Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila, ujenzi wa miundombinu ya hosteli zitakazochukua wanafunzi 1,370, ujenzi wa maktaba, kafeteria, madarasa na ukumbi wa mihadhara utagharimu shilingi bilioni 13.3,” alisema Waziri Mkuu.
0 comments:
Post a Comment