METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 10, 2021

KAMPUNI YA TUMBAKU YABORESHA HUDUMA ZA JAMII

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian akiongea na wakazi wa Vijiji vya Utemini na Maswanya katika kata za Ndono na Kakola wilayani Uyui mkoani Tabora baada ya kuzindua zoezi la upandaji miti katika mashamba ya vyama vya msingi (Amcos).  

Na Lucas Raphael,Tabora

KAMPUNI ya Japan Tobacco International (JTI) inayojishughulisha na ununuzi wa zao la tumbaku Mkoani Tabora imepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutatua kero za jamii Mkoani hapa.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akizindua msimu mpya wa kilimo cha zao la tumbaku kwa kupanda miti katika mashamba darasa ya wakulima katika vijiji vya Utemini na Maswanya vilivyoko katika kata za Ndono na Kakola wilayani Uyui.

Alisema Kampuni hiyo ni mfano wa kuigwa na makampuni mengine ya ndani na nje ya nchi kwani licha ya kutekeleza wajibu wao wa kununua tumbaku kwa ufanisi mkubwa pia wamekuwa wakijitolea kusaidia huduma za kijamii.

Alitoa mfano wa huduma hizo kuwa ni ujenzi wa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa vituo vya afya, visima vya maji safi na ukarabati wa madarasa na nyumba za walimu.

 ‘Nawapongeza sana JTI  kwa kujali wakulima na kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 kwa kuboresha huduma za jamii ikiwemo kujenga miundombinu ya elimu, afya na maji’, alisema.

Dkt Batilda aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa kusimamia ipasavyo zoezi la upandaji miti ambapo hadi sasa zaidi ya miche 10,000 imepandwa katika halmashauri 8 za Mkoa huo.

Alisema kuwa miti husaidia kutunza uoto wa asili na kuboresha mazingira, hivyo akatoa wito kwa makampuni ya tumbaku na wadau wengine kuiga mfano wa JTI, huku akionya wanaoendeleza vitendo  vya kukata miti au kuchoma moto ovyo.

Alibainisha kuwa kilimo cha tumbaku licha ya kutumia kuni nyingi kwenye ukaushaji, wakulima bado wanaongoza kwa vitendo vya ukataji miti ovyo na kuchoma moto hali inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira.

Aliongeza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya miti yote inayopandwa na wakulima inakufa kwa kukosa utunzaji mzuri, hivyo akaagiza viongozi wa ushirika na Amcos kuhakikisha miti wanayopanda inatunzwa vizuri na inakua.

Dkt Batilda aliwataka wale wote wanaovamia maeneo ya hifadhi za serikali na kuanza kufanya shughuli za kilimo kuacha mara moja tabia hiyo ili kuepusha uharibifu wa hifadhi hizo na rasimali zilizomo.

Meneja Kilimo wa JTI Alfadhil Makengo alisema kuwa kampuni hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo hivyo wataendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kutatua kero za wananchi.

Naye Meneja Mwendelezaji wa zao hilo kutoka Bodi ya Tumbaku Tanzania, Osca Simwanza alisema kuwa sheria no.24 ya 2001 inataka kila mkulima kupanda miti ili kukabiliana na uhalibifu wa mazingira.

Aliongeza kuwa Bodi imeendelea kusimamia utekelezaji wa programu zake 2 kwa wakulima ambazo ni upandaji miti ili kulinda mazingira na kuhamasisha matumizi ya majiko banifu ya kisasa ya kukaushia tumbaku ambayo hayatumii kuni nyingi. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com