METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, August 12, 2020

KATIBU MKUU KILIMO ATILIA SHAKA UWEPO WA RUSHWA KWA VIONGOZI WA KDCU, AWATAKA KUWASILISHA TAARIFA ZAO ZA BENKI TAREHE 30 AGOSTI, 2020

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akisaini kitabu cha Wageni kabla ya kuanza kikao kifupi na Viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akisalimia na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KDCU pamoja na Meneja wake Bwana Oscar Dominick alipofika kwa ajili ya kuwa na mazungumzo na Viongozi na Watumishi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KDCU.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiongoza kikao katika Ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika cha KDCU kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Godfrey Mheluka anayefuata ni Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KDCU Bwana Oscar Dominick.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya leo tarehe 12 Agosti, 2020 ameweka bayana kutilia shaka mienendo ya Viongozi na Watumishi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Karagwe na Kyerwa (KDCU) wakati wa mkutano wake na Viongozi na Watumishi hao katika ukumbi wa makao makuu ya Chama hicho Kikuu, wilayani Karagwe.

Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya amesema katika taarifa za awali kutoka kwa wasamalia wema zimeonyesha kuwa kuna tuhuma; Kuwa kuna baadhi ya Wanunuzi wa kahawa, wamekuwa wakitoa rushwa ili wauziwe kahawa kwa bei ya chini; Jambo ambalo linachangia kuwadhulumu Wakulima haki yao ya kupata bei nzuri.

Katibu Mkuu Kilimo Bwana Kusaya amemtaja Mnunuzi mmoja wapo kuwa ni Mmiliki wa Kampuni ya Mambo Coffee; Kuwa amekuwa mstali wa mbele katika utekelezaji wa jambo hilo.

Bwana Kusaya ameongeza kuwa kwa nyakati tofauti Viongozi na Watumishi wa KDCU wamekuwa wakipokea fedha kwa njia ya simu na kwenye akaunti zao za Benki, Ikidhaniwa kuwa ni kwa ajili ya kutekeleza nia ovu ya kushawishi na kutoa upendeleo kwa Wanunuzi binafsi.

Katibu Mkuu Kusaya alimtaja Mhasibu Mkuu wa KDCU Bwana Juvenary Burchard, Mtumishi mwengine ni Bwana Oscar Dominick Mjuni aliwekewa fedha kiasi cha shilingi milioni 1 saa 2:07 usiku wa tarehe 12 Machi, 2020 na tarehe 14 Machi, 2020 aliwekewa tena kiasi cha shilingi milioni 1, Mtumishi mwengine aliyefahamika kwa jina moja Bi. Whitney ambapo, tarehe 1 Aprili, 2020 saa 8:01 mchana aliwekewa kiasi cha shilingi milioni 2.4.

Watumishi hao watatu kwa nyakati tofauti walipoulizwa fedha hizo zilitumwa kwako kwa lengo gani; Wote hawakusema.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo pia haikumuacha salama Mkuu wa wilaya ya Karagwe Mhe. Godfrey Mheluka ambaye naye kwa wakati mmoja alipokea fedha kiasi cha shilingi milioni 1 kutoka kwa Mnunuzi wa kahawa wilayani humo na hata alipoulizwa lengo la kutumiwa fedha hizo na hakusema fedha hizo alitumiwa kwa lengo gani.

Katibu Mkuu Kusaya aliagiza Viongozi na Watumishi hao wa KDCU kuwasilisha taarifa zao za Benki (Bank Statements) kuanzia Januari, 2020 hadi Mwezi Agosti, 2020 na kwamba zimfikie ofisini kwake Dodoma tarehe 30 Agosti, 2020.

Awali Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya alitaka kufahamu taarifa ya kupotea kwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.7; Akijibu swali la Bwana Kusaya, Meneja wa KDCU Bwana Oscar alianza kwa kusema fedha zilizopotea ni shilingi bilioni 3.4 na si 5.7 na kuendelea kumfahamisha Katibu Mkuu kuwa ufisadi huo ulitokea mwaka 2014 na kuongeza kuwa hii ni Bodi ya Viongozi wa Awamu ya Nne na kwamba  hawahusiki na kutoa maelezo kuwa  usahihi wa deni hilo unaweza kufahamika kuanzia mwaka 2014 kurudi nyuma.

Katika hatua nyengine Katibu Mkuu Kusaya alidokeza kuwepo kwa taarifa za kutia shaka kuhusu uwezo wa kifedha wa Meneja wa KDCU Bwana Oscar Dominick ambapo kuna tuhuma kuwa anamiliki hotel inayojulikna kwa jina la Toronto.

“Kuna taarifa kuwa Bwana Oscar unamiliki hotel inayoitwa Toronto, wewe kama Kiongozi wa Umma naamini ulijaza fomu ya tamko la mali; kila kila sababu ya kuulizwa na kudhibitisha ulipata wapi hizo fedha za kujenga hiyo hotel, kabla ya kuwa Kiongozi wa KDCU au ulizipata wakati ulipokuwa Kiongozi na ulizipataje?.” Amekaririwa Bwana Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya wakati wa mazungumzo yake aliuliza kuhusu ukaguzi uliopita kwa Chama hicho Kikuu cha KDCU ambapo Bwana Oscar Dominick alisema Chama kilipata hati yenye mashaka na kusema sababu kuwa ni kuchelewa kuwasilisha taarifa ya benki (Certified Bank Statement) ambayo ingeonyesha kama Chama hiko Kikuu ch Ushirika kilimaliza kulipa deni lake kutoka Benki ya Kilimo (TADB). Fedha hizo zilikopwa ili kulipa madeni ya Wakulima wa zao la kahawa.

Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amewaonya Viongozi wa Chama Kikuu cha KDCU na kuwakumbusha maneno ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kaasim Majaliwa kuwa; kama kuna Kiongozi ambaye amechaguliwa kuwa Kiongozi kwenye Chama cha Ushirika akiamini kuwa kwa kuwa atawaibia Wanachama na akatajirika haraka haraka, aache mawazo hayo. Ushirika wa sasa hautawavumilia Viongozi wezi na wabadhilifu.

Aidha katibu Mkuu amewaagiza Viongozi wa Chama Kikuu cha KDCU kuanza mara moja mchakato wa kununua mizani bora na ya kisasa kwenye AMCOS ili kuondoa kero ya Wakulima kulalamikia kuibiwa mazao yako.

“Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa Wakulima kwenye zao la kahawa na korosho, wanapopima kwenye AMCOS zao na baadae wanapopeleka kwenye Chama Kikuu kuna kuwa na utofauti wauzito, hatuihitaji tena kusikia tofauti za mizani”

Nafaham KDCU ina AMCOS zaidi ya 100; Anzeni kununua kwa awamu  baadae mtakuwa mmetimiza lengo la kununua mizani kwa AMCOS zenu zote.

“Wito wangu kwenu KDCU pangeni mipango vizuri na hakikisheni msimu wa ununuzi wa zao la kahawa; mnalipa madeni yote ya Wakulima, ingie msimu mwengine bila ya kuwa na madeni, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hataki kusikia kero za aina hii”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com