Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula akijadiliana na wataalamu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania akiwa kwenye kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano cha Namanga, Arusha
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga
akinyoosha mkono kwenye betri za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye kituo
cha Mananga, Arusha wakati wa ziara ya kukagua miundombinu huo. Wa pili kushoto
ni Dkt. Zainabu Chaula, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wa Sekta ya Mawasiliano
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula, jana amefanya ziara ya kukagua miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika mkoa wa Arusha. Hii ni ziara yake ya kwanza ya kukagua miundombinu hiyo tangu alipoteuliwa kuongoza Sekta hiyo ambapo ukaguzi huo utamuwezesha kusimamia vema Sekta hiyo
Dkt. Chaula akiwa ziarani mkoani humo, amebaini nguvu ya miundombinu huo katika kuendesha shughuli za Serikali na kuhudumia wananchi ambapo taaasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi wanatumia miundombinu na huduma za mawasiliano katika masuala ya kiuchumi na kijamii
“Sekta ya Mawasiliano ni Sekta ya uchumi, kimkakati, mtambuka na wezeshi na Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 630 kujenga miundombinu huo”, amesisitiza Dkt. Chaula. Ameyasema hayo wakati alipokutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega walipofika ofisini kwake kabla ya kuanza ziara ya kukagua muundombinu huo
Naye Kwitega alimueleza Dkt. Chaula kuwa taasisi za Serikali zinatumia miundombinu huo pamoja na huduma za mawasiliano kwa kiasi kikubwa ikiwemo uendeshaji wa mifumo mbali mbali ya Serikali ya ukusanyaji wa mapato, utoaji wa huduma kwa wananchi na malipo mbali mbali kwa watumishi wa umma na wadau na amesema kuwa Sekta hii inategemewa na Serikali na wadau wake
Kaimu Meneja wa TTCL Mkoa wa Arusha, Emmanuel James amemweleza Dkt. Chaula kuwa katika Mkoa huo, TTCL wana wateja wa aina mbali mbali ikiwemo taasisi za Serikali, sekta binafsi mfano benki, kampuni za simu, hospitali, shule; huduma mtandao mathalani malipo mtandao kama vile kulipia huduma za maji na umeme; ada; ukusanyaji wa mapato, kodi na tozo mbali mbali; huduma za afya mtandao, elimu mtandao na biashara mtandao
Wakiwa ziarani humo kwenye kituo cha miundombinu huo, Namanga, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wa Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga ameulinganisha Mkongo huo na miundombinu ya barabara kwa kuwa Mkongo huo unabeba na kusafirisha mawasiliano ya data na sauti na kupeleka kwa wateja ambapo Serikali imejenga vituo tisa mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ili kuweza kuzipatia nchi jirani huduma ya mawasiliano
Dkt. Chaula amesema kuwa Serikali inategemea sana miundombinu ya Mkongo wa Taifa Mawasiliano katika kuendesha shughuli zake na kuhudumia wananchi hivyo ametoa rai kwa TTCL kuendesha miundombinu huo kwa maslahi ya taifa.
0 comments:
Post a Comment