Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela mapema leo amewachapa viboko wanafunzi watano waliohusika katika tukio la kuchoma moto shule ya sekondari ya Wavulana ya Oswe na kusababisha hasara ya Zaidi ya shilingi milioni 26.
Brig. Jen. Mwangela amefikia hatua hiyo mara baada ya kamati aliyoiunda ya kuchunguza chanzo cha ajali ya moto uliotokea shuleni hapo Julai 3 mwaka huu kubaini kuwa wanafunzi wawili Naftari Nganga na Collin Kisinga ndio waliochoma mabweni ya shule hiyo huku wenzao watatu wakiwa na taarifa za mipango hiyo na hawakuripoti.
Amesema wanafunzi hao walianza mpango wa kuchoma moto mabweni mnamo Juni 28 kwa kununua vifaa vya kuchomea, ilipofika Julai 2 walijaribu kuchoma bweni lakini halikuwaka, Julai 3 walichoma bweni likawaka na kusababisha hasara hiyo na Julai 6 walifanya jaribio lingine tena la kuchoma moto ghala la chakula lakini halikuwaka moto.
Brig. Jen. Mwangela ametoa miezi mitatu kwa wazazi wa Naftari na Collin kila mmoja alipe shilingi milioni 7.3, Mmiliki wa Shule pia alibainika kuwa na uzembe wa kuweka vifaa vya kuzimia moto hiyo alipie shilingi milioni 7.3 huku mwalimu wa zamu siku ya tukio, mlinzi na Patroni nao wakitakiwa kulipa shilingi milioni 4 ili kufidia hasara iliyotokana na ajali hiyo ya moto.
Aidha Brig. Jen Mwangela amewaagiza maafisa elimu wote Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika shule zote ili kubaini endapo elimu ya tahadhari ya majanga ya moto na vifaa muhimu kwa ajili ya kuzima moto vimewekwa katika maeneo ya shule pamoja na kuzingatia taratibu na miongozo ya uendeshaji wa shule.
Pia amewataka wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha tabia za kujiingiza katika vitendo viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao kwani taifa linawategemea wawe wananchi bora na viongozi au watendaji wa baadae.
Mama mzazi wa mwanafunzi Collin aliyechoma moto shule Bi Agnes Kisinga amesema kitendo alichofanya mwanafunzi huyo si kizuri na amesikitishwa sana huku akitoa wito kwa walimu kushirikiana na wazazi katika malezi huku akiwaasa wanafunzi kuzingatia masomo.
Naye Mwanafunzi Denis Petro wa kidato cha tatu katika shule hiyo amesema tukio hilo limewasababishia hasara kwa kuwa vifaa vya shule viliteketea kwa moto huku akiwaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha matendo mabaya kama ya kuharibu mali za shule.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Wavulana ya Oswe Fabian Mwalyego amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa kuchukua hatua muhimu katika kukabiliana na janga la moto lililotokea shuleni hapo huku akiahidi kurekebisha mapungufu yaliyobainika katika shule hiyo.
0 comments:
Post a Comment