Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (katikati) pamoja na
ujumbe aliyoambatana nao wakiwa katika kikao cha ndani katika ofisi za kampuni
ya umeme ya TEXPOL iliyopo wilayani Uyole Mkoani Mbeya, walipofanya ziara ya
kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4,2020.
Miongoni
mwa nyumba zilizounganishiwa umeme na kampuni ya umeme ya TEXPOL iliyopo
wilayani Uyole Mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati pamoja na
ujumbe wake walifanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme iliyofanywa
na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4,2020.
Muonekano
wa miundombunu ya umeme iliyosimikwa na kampuni ya umeme ya TEXPOL kwa ajili ya
kusambaza umeme kwa wananchi wa Wilaya ya Uyole Mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu
Wiraza ya Nishati pamoja na ujumbe wake walipofanya ziara ya kukagua kazi ya
usambazaji wa umeme iliyofanywa na kampuni hiyo katika vijiji sita vya wilaya hiyo, Julai 4,2020.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja amesema kazi ya kusambaza
umeme iliyotekelezwa na Kampuni ya TEXPOL katika Kaya zaidi ya mia tatu za
Vijiji sita vilivyopo katika Kata ya Ilungu, Wilaya ya Uyole mkoani Mbeya
haridhishi.
Mhandisi
Masanja alisema hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme
iliyofanywa na kampuni hiyo kwa lengo la kuona, kujiridhisha na kutathmini
ubora wa kazi na miundombinu iliyotumika katika kutekeleza kazi ya usambazaji
umeme katika eneo husika.
Awali,
Kampuni hiyo ilitakiwa kujenga kituo kidogo cha kufua umeme kwa kutumia
maporomoko ya maji katika wilaya hiyo na baadaye kuwauzia wananchi umeme huo
kwa bei elekezi ya serikali, jambo ambalo halikuweza kutekelezwa hadi sasa.
Badala yake kampuni hiyo ilifanya kazi ya kusambaza umeme kama zinavyofanya
kampuni zingine katika mradi wa usambazaji umeme vijijini katika maeneo
mbalimbali nchi.
Ziara hiyo
ilifanyika, Julai 4, 2020, ambapo Naibu Katibu Mkuu huyo aliambatana na
Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Viongozi wengine kutoka
Taasisi zilizochini ya wizara hiyo ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji,
(EWURA) ili kila mmoja aweze kuona namna ambavyo kampuni hiyo imetekeleza kazi
zake kwa kiwango na kwa kuzingatia vigezo na ubora unayotakiwa.
Baada ya
ziara hiyo, changamoto na dosari mbalimbali zilionekana katika kutekeleza mradi
huo, hivyo Mhandisi Masanja aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO),
kuwasilisha taarifa inayoeleza mchakato mzima wa utendaji kazi wa kampuni hiyo
na namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana katika kazi.
Katika hali
isiyokuwa ya kawaida, uongozi wa juu wa kampuni hiyo haukuweza kushiriki ziara
hiyo licha ya kupewa taarifa juu ya ziara hiyo katika eneo lao la kazi,
kutokana na sababu mbalimbali, hata hivyo walimuagiza mmoja wa wahandisi
aliyejulikana kwa Jina la Chakuja ili kushiriki ziara hiyo, ambaye pia hakuweza
kujibu baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa kwakuwa hakuwa na majibu.
“Hii ziara
inafahamika na uongozi wa kampuni ya TEXPOL unafahamu na wamekuwa wakiwasiliana
na Kamishna msaidizi, cha ajabu hawapo eneo la tukio ili tuweze kuwauliza
maswali yetu na kupata majibu stahiki, badala yake wamemuagiza huyu kijana
mhandisi ambaye hawezi kutupatia majawabu stahiki na hafahamu, TANESCO mtaleta
taarifa ya maandishi Wizarani kwakuwa ninyi ndiyo mnawasimamia na mnawafahamu
vyema,”alisema Mhandisi Masanja.
Vijiji
vilivyounganishiwa umeme na kampuni hiyo katika kata hiyo ya Ilungu iliyopo
Wilaya hiyo ya Uyole ni Mwela, Ifupa, Mashese, Nyalwela, Ngole pamoja na
Shango, ambavyo vina Kaya zaidi ya mia tano, mia tatu kati ya hizo tayari
zimeunganishiwa umeme, zikiwemo baadhi ya shule na vituo vya afya.
Kwa upande
wake mwakilishi wa kampuni ya TEXPOL, aliueleza ujumbe wa ziara hiyo kuwa bado
kampuni hiyo ipo katika mchakato wa kujenga kituo kidogo cha kufua umeme kama
ilivyoelezwa hapo awali, kinachosubiriwa sasa ni fedha walizoziomba kutoka kwa
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambazo wanategemea kuzipata.
Hata hivyo
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alimueleza
mwakilishi huyo kuwa, kampuni hivyo haiwezi kupata fedha hizo kwa sababu
haikuweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa, vilivyoweka katika ushindani wa kuomba
fedha hizo ikiwa pamoja na kushindwa kukamilisha kazi za awali.
Vilevile
tayari kampuni hiyo imeandikiwa barua ya kufahamishwa juu ya kilichotokea.
0 comments:
Post a Comment