METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 14, 2020

COSOTA YAHAMIA RASMI WIZARA YA HABARI


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe akisisitiza kuisimamia COSOTA kuandaa mikataba kati ya nchi na nchi ili wasanii wamuziki waweze kunufaika na kazi zao zinazopigwa katika vyombo vya habari  nchi ya nje, kwa kupata gawio kwa lengo la kulinda hakimiliki ya kazi zao, leo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusaini waraka wa kuhamishia ofisi hiyo ndani Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Julai 13,2020.


Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ameeleza kuwa lengo la kuihamisha Taasisi ya Hakimiliki (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kuja katika Wizara anayoisisimamia ni kuhakikisha wadau wa Sanaa wanapata huduma sehemu moja  kwa sababu asilimia 86% ya wadau wake ni Wasanii.


Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dodoma katika Mkutano na Waandishi wa habari ambapo amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli jana tarehe 13/07/2020 amesaini Waraka unaogawa majukumu kwa wizara kuruhusu mabadiliko hayo muhimu ambayo yanawagusa wabunifu,watunzi  waandishi wa vitabu,kazi za Sanaa na Sanaa na jadi.

“Namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hii ndani ya saa ishirini na nne awe amekutana na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ili waweze kukabidhiana nyaraka muhimu za uendeshaji wa COSOTA”alisema Dkt.Mwakyembe.

Aidha Waziri huyo ameeleza kuwa ujio wa COSOTA katika Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo utarahisisha ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) katika kulinda na kusimamia maslahi ya wasanii wa filamu na muziki pamoja na kupanua wigo wa malipo na stahili za wasanii kwa kazi zao katika majukwaa mbalimbali ya Sanaa kielektroniki.

Mhe.Waziri amesisitiza kuwa lazima COSOTA ya sasa iingie mikataba na nchi za nje ambazo vyombo vyake vya habari vimekua vikipiga muziki wa wasanii wa Tanzania bila kuwapatia gawio au kufaidika kwa namna yoyote ile.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com