Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe amesema Jumuiya ya maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC) imeendelea kutambua mchango mkubwa wa wanahabari kwa nchi
wanachama wa ukanda huo.
Akizungumza
katika Ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Kutafuta Washindi wa tuzo za Wanahabari
wa Habari za SADC uliofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha
Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Waziri Mwakyembe alieleza kuwa uongozi wa
SADC chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli unaendelea
kuwathamini waandishi wa habari katika ukanda huo wa Afrika.
“SADC
chini ya uenyekiti wa Mhe, Dkt. Magufuli inaendeleza utamaduni wake wa kutambua
mchango mkubwa wa wanahabari katika nchi wanachama sio tu katika kuandika
habari njema za SADC kama vile za
utekelezaji miradi ya maendeleo na sera bali pia katika kuelimisha na
kuhabarisha wanachi wakati wa majanga mbalimbali yakiwemo ya milipuko ya
magonjwa, vimbuga, vurugu katika jamii,
ukame pamoja na uvamizi wa nzige”, Alisema Dkt. Mwakyembe.
Alisema
kuwa waandishi wa habari wametumia vyema njia mbalimbali za kutoa habari
zikiwemo mitandao ya kijamii, Redio, Televisheni na Magazeti katika kutekeleza
majukumu yao ya kusambaza taarifa sahihi na za kweli kwa umma kuhusu mwenendo
wa ugonjwa wa Covid-19 uliozikumba nchi za ukanda wa SADC, kwani kazi hiyo ya
kuelimisha wananchi ukanda wa SADC imekuwa nzuri na inapaswa kuthaminiwa kwa
nchi zote za SADC.
Waziri
Mwakyembe aliwashukuru waandishi wa habari kwa kutekeleza majukumu makubwa ya
kuwahabarisha wananchi katika Mkutano Mkuu wa
39 wa Wakuu wa Nchi za SADC
uliofanyika mwezi Agosti mwaka jana na kuhudhuliwa na wakuu wa nchi
wanachama takribani 16.
“Napenda
kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa waandishi wa habari wote
walioshiriki kutoa taarifa za Mkutano sa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za
SADC, uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Tanzania Mwezi Agosti mwaka jana”,
Alisema Dkt.Mwakyembe.
Aidha,
Dkt.Mwakyembe ameipa kamati hiyo muda wa siku mbili ili kuweza kuwapata
washindi wa tuzo hizo ambapo kamati hiyo imepokea kazi za magazeti 9, Televisheni 5, Redio 8 na picha 6, na ameitaka kamati hiyo kuchakata
majina hayo kwa umakini na weledi mkubwa ili kuwezesha upatikanaji wa washindi
wenye kazi bora.
Kwa
Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa mpaka sasa kazi zilizopokelewa na kamati hiyo
zinakidhi kuingia katika ushindani ambao kila mmoja ataweza kupata nafasi ya
kushindana na ubora wa kazi yake baina ya washiriki kutoka ukanda huo wa
Afrika.
“Mpaka
sasa kazi zilizopokelewa na ambazo zitafanyiwa mchakato ni kazi 28 amabapo kazi
za magezeti ni 9, Televisheni kazi 5, Redio kazi 8 na picha 6 na kazi hizi
zimepokelewa kutoka nchi mbalimbali wananchama wa SADC, kwa hiyo kamati ipo
kutekeleza jukumu la kutupatia washindi wenye kazi bora kwa kuwa kazi zote
zimekidhi ushindani”, Alisema Dkt.Abbasi.
Jumuiya
hiyo ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), inatimiza miaka 40 tangu
kuanzishwa kwake na kuziweka nchi 16 za ukanda huo wa Afrika kuwa na
ushirikiano katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment