METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, May 5, 2020

WANANCHI WA KIJIJI CHA IGAWA WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA


Barabara ya Igawa-Mafinga ikiwa katika mwonekano wa sasa mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kufanya maboresho mbalimbali ya miundombinu ya barabara hiyo ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani. 
WANANCHI wa Kijiji cha Igawa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wamempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha miundombinu ya barabara hatua inayolenga kufungua fursa za kiuchumi na ukuaji wa miji katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO) hivi karibuni Kijijini hapo, wananchi hao walisema udhubutu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara utaacha alama ya kihistoria kwa vizazi vijavyo kuhusu wajibu wa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
Bw. Christom Variyamba Mkazi wa Kijiji cha Igawa alimpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa udhubutu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutengeneza barabara nyingi zenye viwango vya kimataifa katika kipindi kifupi ikiwemo barabara ya Igawa-Mafinga, na kutoa fursa kwa wananchi kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo.
‘’Kwa sasa Dar es Salaam tunafika kwa wakati na salama kabisa, barabara hii ya Igawa-Mafinga imejengwa kwa miundombinu ya kisasa kabisa ikiwemo mataa ya barabarani na hii itasaidia kupunguza ajali wakati wa usiku kwani iwapo kutatokea gari likapata tatizo wakati huo utaweza kuliona’’ alisema Variyamba.
Naye Bw. Hamadi Nuru anasema awali Kijiji cha Igawa hakikuwa na maendeleo, lakini hali ni tofauti kwa sasa kwani ujenzi wa barabara katika Kijiji hicho kumeweza kutoa hamasa ya wananchi kushiriki katika shughuli za biashara wakati wa biashara na hivyo kuwaongezea kipato kutokana na uwepo ya taa za kisasa zilizofungwa katika barabara hiyo.
Kwa upande wake Bi. Rehema Ally anasema Igawa ya sasa si ile ya zamani, kwani Kijiji hicho cha sasa kinakua kwa kasi na kukimbizana na Miji mikubwa nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, hatua inayowalazimu wakazi mbalimbali kutoka Mikoa mbalimbali nchini kurejea katika Kijiji hicho kuweza kutumia fursa ya miundombinu ya barabara hiyo kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
‘’Mimi binafsi niliondoka Igawa kwa muda mrefu lakini niliporejea mwaka 2019 niliona hali ni tofauti kabisa, mji umekuwa, biashara zimeshamiri na hiyo inatokana na maboresho makubwa ya barabara ya Igawa-Mafinga, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na jitihada kubwa inazofanya katika kusogeza huduma muhimu kwa wananchi wake’’ alisema Rehema.
Mwananchi mwingine Mkazi wa Igawa, Rehema Kwila alisema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano Kijiji cha Igawa na wananchi wake wameshuhudia mageuzi makubwa ya huduma za kijamii ikiwemo barabara ambazo zimesaidia kuondoa changamoto za muda mrefu ambazo zilishindwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
‘’Tangu kuingia kwake madarakani  Rais Dkt. John Magufuli mambo mengi yamebadilika, kwani uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa sana katika Kijiji chetu cha Igawa, barabara zimeboreshwa kwani awali kulikuwa na mashimo mengi barabarani hali iliyotulazimu kutumia masaa matatu-manne kufika Makambako’ alisema Kwila.
Naye Bw. Aloyce Peter, Dereva wa magari makubwa yaendayo Nje ya Tanzania, anasema kwa sasa wanatumia siku 2 kutoka Dar es Salaam hadi mpaka Tunduma, Mkoani Songwe ikilinganishwa na hapo awali ambapo katika kipande cha barabara ya Igawa-Mafinga hali haikuwa nzuri kwani walikuwa wakitumia masaa takribani 8 na siku nne kufika eneo la mpaka wa Tunduma.
Anasema miundombinu ya barabara za Tanzania ni nzuri ikilinganishwa na nchi anazosafiri za Zambia Congo ambazo nyingi zina mashimo na kusababisha kusafiri kwa umbali mrefu kutoka katika eneo la Mpaka wa Tunduma huku magari hayo yenye uzito wa tani 30 yakilazimika kusafiri kwa takribani masaa 12 kufika katika miji mikuu ya nchi hizo.

‘’Miundombinu ya barabara za Tanzania imeboreshwa sana, kwa nchi nyingine tunazokwenda barabara zao siyo nzuri, kwa mfano kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma tunatumia muda mfupi sana wa siku 2, lakini hali ni tofauti sana tunapokwenda katika barabara za mataifa jirani, miundombinu yao siyo imara kama ilivyo hapa nyumbani Tanzania’’ anasema Peter.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com