METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, April 14, 2019

MAJALIWA AFUNGUA MICHUANO YA AFCON U17

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi katika mechi ya ufunguzi wa Michuano ya AFCON  U17 ambapo Tanzania  ilipambana na Nigeria kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Aprili 14, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiikagua Timu ya Tanzania ya  Serengeti Boys  iliyopamba na Nigeria katika  mechi ya Ufunguzi wa Michuano ya AFCON U17 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Aprili 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua  Mashindano ya AFCON U17 kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam Aprili 14, 2019. Wenye Jezi za Bluu ni Timu ya Tanzania – Serengeti Boys na kulia ni Timu ya Nigeria. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua mashindano ya AFCON U17 na kutangaza kuwa kuanzia kesho Watanzania wataingia bila kulipia.

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumapili, Aprili 14, 2019) kwenye ufunguzi wa michuano hiyo iliyoanza leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa michuano hiyo, aliambatana na Rais wa Shirikisho la Soka na barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad kukagua timu zilizofungua dimba na kisha akatangaza uamuzi huo wa Serikali. 

Timu zilizofungua dimba leo ni Serengeti Boys ya Tanzania na Nigeria. Katika mchezo wa leo Nigeria imeibuka kidedea baada ya kuifunga Tanzania mabao 5-4. Hadi mapumziko timu ya Nigeria ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-1.

Mabao ya Nigeria yalipatikana dakika ya 20, 29, 36, 71 na 78 wakati mabao ya Tanzania yalipatikana dakika ya 21, 51, 56 na 60 ambapo magoli mawili kati ya hayo, yalipatikana kwa njia ya penati.

Bao la kwanza la Tanzania lililofungwa na Alphonce Mabula Msanga lilitinga kimiani dakika ya 21. Bao la pili, lilipatikana dakika ya sita ya kipindi cha pili na lilifungwa na Kelvin Pius John.

Dakika tano baadaye, Morice Michael Abraham aliipatia Tanzania bao la tatu lililofungwa kwa njia ya penati. Kabla vijana wa Nigeria hawajakaa sawa, dakika nne nyingine, Edmund Godfrey John alitinga kimiani bao la nne, ambalo pia lililifungwa kwa penati.

Timu ya Tanzania iko kundi A na imepangwa na timu za Nigeria, Uganda na Angola. Michuano hii inatarajiwa kumalizika Aprili 28. Endapo timu hiyo ya Taifa ya vijana ya Serengeti Boys itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili, itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia kwa vijana wa umri wa miaka 17 yatakayofanyika mwakani huko Brazil.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com