Mafundi
wakiendelea na kazi ya ujenzi wa nguzo kubwa za kusafirisha umeme utakaotumika
katika reli ya kisasa(SGR) kuendesha treni ya umeme, Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani alifanya ziara ya kukagua njia ya kusafirisha umeme Mei 11,
2020 mkoani Morogoro.
Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati)akipata maelezo kutoka Msimamizi Mkuu
wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa utakaotumika katika reli ya
kisasa(SGR) kuendesha treni ya umeme wakati alipofanya ziara ya kukagua njia
hiyo, Mei 11, 2020 mkoani Morogoro.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(
katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Umeme wa Kiwanda cha
Sukari Mtibwa, wakati Waziri alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho
kufahamu hali ya upatikanaji wa umeme, Mei 11, 2020 mkoani Morogoro.
Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha
umeme utakaotumika katika Reli ya kisasa ya kuendesha Treni inayotumia umeme
umekamilika kwa zaidi ya asilimia 94 na utakamilika mwishoni mwa mwezi Mei
2020.
Dkt.
Kalemani alisema hayo mkoani Morogoro , alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa
miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme mkubwa, na kusema kuwa ameridhishwa na
kasi ya ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu pamoja
na kutembelea Kiwanda cha Sukari Mtibwa kuona hali ya upatikanaji wa umeme.
Alisema
Kukamilika kwa mradi huo kutachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa
kuongeza mapato kwa kuwa umeme mwingi utakuwa ukinunuliwa kutoka Shirika la
Umeme nchini (TANESCO), vilevile Shirika la Reli nchini( TRL) litapunguza
gharama za kununua mafuta ya kuendesha treni.
Njia hiyo
ya umeme itapita katika vituo vinne vya njia ya treni ya kisasa ambavyo ni Pugu
mkoani Dar es salaam, Ruvu mkoani Pwani, Kidugaro na Kingulwira mkoani
Morogoro.
“Mradi huu
utakamilika ndani ya muda uliopangwa, kwa sababu tayari nguzo kubwa za umeme
450 kati ya 455 zinazotumika katika ujenzi wa njia hiyo, zimekwisha jengwa na
kusalia nguzo tano(5) tu ambazo zinaendelea kujengwa ili kukamilisha ujenzi,
hivyo kabla ya mwisho wa mwezi huu, mkandarasi atakuwa amemaliza kazi yote, na
kitakachofuata ni kusubiri kukamilika kwa reli yenyewe ili tuanze kufanya
majaribio ya umeme huo”, alisema Dkt.Kalemani.
Alisema
kuwa mradi huo ni wa kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki,ukifuatiwa na Kenya
ambayo imepanga kuanza kuujenga mwakani 2021,na Uganda ambayo imepanga kuanza
kujenga mwaka 2025.
Mradi huo
umegharimu zaidi ya shilingi za kitanzania Bilioni 72.6, na mkandarasi amekuwa
akilipwa fedha zake kwa wakati.
Akiwa
katika Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Dkt. Kalemani alisema kuwa serikali imetenga
shilingi za kitanzania Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha
umeme utakaokuwa ukitumiwa na kiwanda cha sukari peke yake, katika kuendesha
shughuli za uzalishaji.
Njia hiyo
ya umeme inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita kuanzia mwezi Mei mwaka
huu, ambayo itasaidia kiwanda hicho kupata umeme mwingi na kutosha kukidhi mahitaji
ya kiwanda na ziada kwa zaidi ya miaka mitano ijayo.
“Kilichonileta
hapa ni kuwajengea njia ya umeme wenu peke yenu, tumeshakaa na wataalam ili
kumaliza tatizo hili, umeme hapa unatoka Msamvu takribani Kilomita 100 na
unatumiwa na watu wengi, fedha tayari imekwisha tengwa na ujenzi utanza
keshokutwa (Mei 13,2020) ili kukidhi mahitaji yenu ya kutaka umeme takribani
Megawati 27 kwa miaka 5 ijayo, sasa lazima tuwape zaidi bila shaka mtatanua
kiwanda hichi hapo baadaye,” alisema Dkt. Kalemani.
Kwa sasa
kiwanda cha sukari Mtibwa kinapata Megawati 5 hadi 8 ambao pia wakati mwingine
unakuwa na nguvu ndogo kutokana na kusafiri umbali mrefu pia umekuwa ukikatika
kusababisha uharibifu wa vifaa na kutokidhi mahitaji ya uzalishaji.
Kiwanda
hicho lilijengwa mwaka 1954 na kuanza uzalishaji mwaka 1963 hadi sasa,
kinauwezo wa kuzalisha tani 200 hadi 35 za sukari kwa siku, matarajio ni
kuzalisha tani 1000 kwa siku kwa kuwa wanafanya ukarabati na kuboresha
miundombinu kiwanda hicho ikiwemo umeme.
0 comments:
Post a Comment