Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akisoma
tamko juu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, mbele ya waandishi wa
Habari hii leo Jijini Dodoma. Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kwa
kutumia vyombo vya habari bila kuwapo kwa mikusanyiko.
Serikali imesema kuwa mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa yaliyopangwa kufanyika
Mkoani Lindi tarehe 5 Juni 2020 hayatafanyika kutokanana mlipuko wa Ugonjwa wa
Homa ya Mapafu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan katika Mkutano wake na Waandishi wa
habari uliofanyika Jijini Dodoma.
“Kama
mnavyofahamu, Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya watu. Uwepo
wa janga hili umesababisha kusitishwa kwa shughuli zinazohusu mikusanyiko ya
watu wengi.” Zungu alisisitiza.
Kwa
muktadha huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo wamekubaliana kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani
yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari
pamoja na mitandao ya kijamii
kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na
maambukizi ya ugonjwa wa corona.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Mazingira ambao
ni UNDP, UNEP, WWF, GIZ, Forum CC, Vodacom Foundation,
USAID, nchi wahisani pamoja na vyombo
vya habari tunahamasisha na kuelimisha jamii kukabiliana na athari za
mabadiliko ya Tabianchi kwa kuhifadhi Mazingira hivyo kutakuwa na mashindano
ya kuandika insha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mikutano ya kitaalamu
itakayofanywa kwa njia ya mitandao kwa kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha
na maambukizi ya ugonjwa wa Corona” Zungu alisema.
Waziri
Zungu ameikumbusha jamii kuwa hifadhi ya mazingira si kazi ya Serikali pekee
yake bali ni jukumu la kila mmoja katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kaya na
ametoa wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia
kusaidia katika kuhifadhi mazingira.
“Watendaji
wote katika ngazi zote hatuna budi kushirikiana katika kutekeleza kwa ukamilifu
Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira. Kila mmoja ana wajibu na fursa muhimu
katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira hapa nchini.
Ningependa kusisitiza kuwa tushirikiane katika kufanya jitihada mbalimbali ili
kupambana na uharibifu wa mazingira kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukabiliana
na athari za mabadiliko ya tabianchi.” Waziri Zungu alisisitiza.
Amesema
kila mwananchi akiwajibika katika nafasi yake, tutalinda mazingira yetu na
jamii kwa ujumla. Hivyo, shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira
hapa nchini mwaka huu pamoja na mambo mengine, zitalenga kuhamasisha jamii
kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na
kuelimishana jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Kila tarehe 5 Juni, nchi yetu huungana na mataifa mengine
duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani
kitaifa yalipangwa kufanyika mkoani Lindi na Kauli mbiu ya maadhimisho haya
kitaifa ni Tuhifadhi Mazingira: Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi.
0 comments:
Post a Comment