METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, May 4, 2020

RC WANGABO AAGIZA “SPECIAL AUDIT” HUKU ZAIDI YA MILIONI 660 KUTOFAHAMIKA MATUMIZI YAKE KATIKA UJENZI HOSPITALI YA WILAYA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) mkoani humo inafanya ukaguzi maalum (special Audit) wa mapato ya ndani na matumizi yake kutokana na zaidi ya shilingi milioni 885 kuwemo mifukoni mwa wadaiwa (defaulters)  wakiwemo watendaji wa vijiji na kata hali mbayo inazorotesha utekelezaji wa mipango ya serikali ikiwemo kushindwa kuchangia 10% ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mh. Wangabo amesema kuwa hatua stahiki zitachukuliwa bila ya ukakasi kwa wale wote wakaobainika kuwa na makosa, na kufafanua kuwa kati ya jumla hiyo ya fedha, shilingi 376,197,050 ni mapato yaliyokusanywa bila ya uthibitisho wa kupelekwa benki kutokana na taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2018/2019 huku Shilingi 509,033,302/= ikiwa ni makusanyo ambayo hayajawasilishwa benki kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi kufikia tarehe 23.4.2020.

Aidha amesema kuwa uwezo wa Halmashauri kutoa huduma na kutekeleza miradi ya maendeleo unategemea mapato yake ya ndani na hivyo ni wajibu wa Halmashauri kuhakikisha inaongeza ustawi wa Maisha ya wananchi na kuongeza kuwa fedha hizo zingeweza kukamilisha maboma ya madarasa ya Shule za Msingi 176 na ya Shule za Sekondari 35 pamoja na maboma ya nyumba za waalimu wa Shule za Msingi 21 na ya Shule za Sekondari 5.

“Kuhusu suala la hawa watu wanaoitwa “defaulters” namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha kuhakikisha ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) anafanya ukaguzi maalum (special Audit) wa mapato ya ndani na matumizi yake ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe bila ya ukakasi wowote, eneo linguine ni vifaa vya ujenzi wa hospitali ya wilaya ambavyo havikukaguliwa na kamati pia havikuingizwa kwenye daftari la vifaa vyenye thatamani ya shilingi 660,063,745/=,”Alisisitiza.

Mh. Wangabo amesema kuwa kutokufanya ukaguzi wa awali wa vifaa na kutoingizwa kwenye daftari la vifaa kinyume na kanuni namba 244 na 245 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) yam waka 2013 inaonesha jinsi ambavyo halmashauri haizingatii kanuni, hivyo kuonesha uwezekano wa kutopokelewa kwa baadhi ya vifaa au vimepokelewa ila havina ubora uliokusudiwa.

Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga itakuwa ya kwanza kufika mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) tarehe 11.5.2020 ambapo Kamati hiyo itapitia taarifa za fedha za halmashauri kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kupitia hoja za halmashauri pamoja na kuchambua na kuhakiki taarifa za mapato na matumizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com