METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 13, 2017

DC MTATURU AKAGUA UJENZI WA UPANUZI WA KITUO CHA AFYA IHANJA

Na Mathias Canal, Wazo Huru Blog

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji J. Mtaturu Leo Disemba 8, 2017 amekagua ujenzi wa upanuzi wa Kituo cha Afya Ihanja ili kujionea hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo.

Akizungumza katika ukaguzi wa ujenzi huo Mhe Mtaturu alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kuboresha huduma za afya kwa wananchi hivyo ujenzi huo ni mahususi kwa ajili ya kurahisisha huduma za utoaji wa afya.

Alisema kuwa Serikali ilitoa shilingi Milioni 500 za ujenzi na Shilingi milioni 220 za vifaa ili kupanua kituo hicho cha afya ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi katika Wilaya ya Ikungi.

Alisema kuwa Ujenzi huo ulioanza Novemba 1, 2017 unatarajiwa kukamalika Februari 1, 2018 na kukabidhiwa ili kutoa huduma bora na huduma nzuri kwa wananchi hao.

Mhe Mtaturu alieleza kuwa Upanuzi huo wa kituo hicho cha afya umelenga kujenga Wodi moja ya Wazazi na watoto, Jengo la upasuaji mkubwa na mdogo, Jengo la maabara, Chumba cha kuhifadhia maiti, Nyumba moja ya mganga, Kichomea taka, miundombinu ya kuvunia maji ya mvua Na chumba cha kufulia nguo na kuanikia.

Aidha, aliitaka kamati ya afya ya kituo hicho cha afya kusimamia vizuri ujenzi ili thamani ya fedha za serikali ionekane na kufanya miundombinu idumu kwa muda mrefu.

Hata hivyo baada ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo hicho cha afya cha Ihanja Mhe Mtaturu aliipongeza kamati ya afya ya kituo hicho sambamba na mafundi kwa kuridhishwa na kiwango cha ujenzi.

Katika hatua nyingine Mhe Mtaturu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Idara ya ujenzi na manunuzi kuhakikisha vifaa vinatolewa kwa wakati ili ujenzi usisimame badala yake kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo Mhandisi Sembua Mrisha alisema kuwa wamejipanga vyema na wanatumia mafundi wa kawaida chini ya usimamizi wao jambo ambalo limesaidia sana kupunguza gharama za ujenzi.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya afya ya kituo hicho cha Ihanja Ndg Leonard Muna alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufanya ziara ya kukagua ujenzi huo huku akiahidi kutekeleza maagizo yote kwa ukamilifu kwa ushirikiano mzuri na kamati ya ujenzi.

Aidha Muna ameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kupanua kituo hicho cha afya kwani baada ya kukamilika kitakuea mkombozi wa sekta ya afya.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com