Waendesha
pikipiki maarufu kama bodaboda wametakiwa kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais
Mhe Dkt John Magufuli ya kufanya kazi
wakati huo huo wakichukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19
unaoenezwa na kirusi cha Corona.
Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula
katika viwanja vya shule ya msingi Buswelu wakati akizungumza na waendesha
pikipiki wa wilaya ya Ilemela juu ya kuchukua tahadhari za maambukizi ya
ugonjwa huo na kukabidhi vifaa vya kujikinga ikiwemo barakoa 1500, vitakasa
mikono katoni 6 na sabuni za kunawia mikono ili viweze kugawanywa katika vituo
vyote vya waendesha pikipiki kwa lengo la kujikinga na maambukizi mapya ya
ugonjwa wa Covid-19
‘.. Suala la magonjwa sio jipya, tulikuwa na ukimwi, tuna malaria, kuna
shinikizo la damu, Sasa hili la Corona lisitufanye tukashikwa na hofu mpaka
tukafa kwa hofu badala ya ugonjwa wenyewe ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula akatumia fursa hiyo kumpongeza Rais Mhe Dkt John
Magufuli kwa kutofunga mipaka ya nchi na kuruhusu wananchi wake kuendelea na
shughuli za kila siku huku wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo sambamba
na kuwataka waendesha pikipiki hao kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa ya
gharama nafuu ICHF ambayo gharama zake ni shilingi elfu 30,000 kwa mwaka
ikiwezesha kuhudumiwa bure katika zahanati na vituo vya afya kwa watu sita
akiwemo baba, mama na watoto wanne
Akimkaribisha mbunge huyo, Mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Ilemela ambae pia
ndie afisa tarafa wa wilaya hiyo Bwana Godfrey Mzava amempongeza mbunge Mhe Dkt
Mabula kwa kazi kubwa anazozifanya katika kuwaletea wananchi maendeleo na hasa
uungaji mkono kwa serikali katika vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 tangu
kuanza kwake ambapo amekuwa akigawa vifaa vya kujikinga kwa makundi mbalimbali
wakiwemo madereva, makondakta, polisi, viongozi wa dini, masoko, vyama vya
siasa, na leo amegawa kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.
Nae Diwani wa kata ya Buswelu ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya huduma ya
manispaa ya Ilemela Mhe Sarah Ng’wani amemshukuru Mhe Dkt Angeline Mabula kwa
juhudi zake katika kuhakikisha anatekeleza shughuli za maendeleo na
kuwasisitiza waendesha pikipiki hao kutunza na kuvitumia vizuri vifaa
vilivyotolewa.
Akihitimisha mwenyekiti wa waendesha pikipiki wilaya ya Ilemela Ndugu Makoye
John Barinago mbali na kushukuru na kumpongeza mbunge huyo kwa msaada wake
alioutoa akamuomba pia kuhakikisha anawasaidia bodaboda hao kupata eneo rasmi
la kufanyia shughuli zao pamoja na kusaidia upatikanaji wa bima ya afya maombi
ambayo yote yalipatiwa majawabu na mbunge huyo papo kwa hapo.
Kupitia zoezi hilo kwa niaba ya mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela Bi Rose Nyemere
alipata fursa ya kuelimisha jamii juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 na
namna ya kujikinga.
0 comments:
Post a Comment