Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa tai) akipata maelezo ya aina za mbegu bora ya pamba zilizogunduliwa na Kituo cha TARI Ukiriguru mkoa wa Mwanza leo.
Watumishi wa chuo cha Kilimo MATI Ukiriguru wilaya ya Misungwi wakimsikiliza Katibu Mkuu ( hayupo pichani) leo alipowatembelea kuzungumza nao.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kushoto) akiwa ameshika muhogo bora unaozalishwa na kituo cha Utafiti wa Kilimo ( TARI) Ukiriguru wakati alipofanya ziara ya kikazi .
Katibu Mkuu Wizara Kilimo Bw.Gerald Kusaya (katikati) akiongea na watumishi wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo MATI Ukiriguru alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa chuo hicho leo wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza.
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)
kupitia kituo cha Ukiriguru mkoani Mwanza imefanikiwa kugundua aina kumi za
mbegu bora za zao la pamba kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima nchini.
Hayo yamebainishwa leo (30.04.2020) na
Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Geofrey Mkamilo wakati akiwasilisha ripoti ya
utendaji kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo alipotembelea kituo hicho
wilayani Misungwi.
Aina mpya za mbegu zilizogunduliwa ni pamoja na
UK 173,uk 08,UK 171 na UK91. Imeelezwa
kuwa mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno tani 2.5 hadi 3.0 kwa hekta na kuwa
na zinahimili ukinzani wa mnyauko fuzari.
Akizungumzia mafanikio hayo Katibu Mkuu Wizara
ya Kilimo alisema wizara inataka kuona mbegu hizo bora zinafikishwa kwa
wakulima wote kwenye mikoa 17 inayozalisha pamba nchini.
Aliongeza kusema watafiti wa mbegu bora
wanapaswa kuendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt.John Pombe Magufuli la kuzalisha mbegu nyingi za pamba na mazao
mengine ili nchi ijitosheleze kwa mbegu.
“ Mikoa 17 nchini inalima zao la pamba na
inataka mbegu bora toka Ukiriguru.Tunahijati mzalishe mbegu nyingi zaidi na
kusambaza kwa wakulima kwa wakati” alisisitiza Kusaya
Takwimu za uzalishaji pamba msimu wa 2019
ilikuwa tani 348,910 kati ya lengo tani
450,000 ambazo ziliuzwa kupitia vyama vya ushirika(AMCOS) na kuingiza shilingi
Bilioni 419.
TARI Ukiriguru imefanikiwa pia kugundua
aina 16 za mbegu za mihogo aina ya
Mkumba,Mkuranga 1,Kizimbani,Kiroba,TARICASSA1,2,3,4 na TARICASS 5 zenye uwezo
wa kutoa mavuno mengi tani
20 hadi 40 kwa hektari na zenye ukinzani wa magonjwa ya CMD na CBSD.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo
ameviagiza Vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini
kuanzisha mashamba darasa bora ya
mazao ili wazalishe na kuuza kwa wakulima lengo ikiwa vijiendesha kibiashara.
Akizungumza na watumishi wa Chuo cha Kilimo (
MATI) Ukiruguru, Katibu Mkuu huyo alisema uwepo wa maeneo makubwa ya ardhi
kwenye vyuo vya mafunzo utumike kuzalisha mazao mengi ya aina tofauti na kuuza kwenye masoko.
“ Nataka tuone namna vyuo vyetu vitaendeshwa
kibiashara kwani uwezo tunao na utaalam upo .Kama mnaweza kufundisha vijana
kilimo cha kisasa na ufugaji kwanini msianzishe kilimobiashara hapa na
kujiongezea kipato ? alihoji Katibu Mkuu
Katibu Mkuu huyo amesema wizara inazo taasisi
za utafiti wa mazao kama TARI na ASA ambazo zinajukumu la kuzalisha mbegu
,hivyo vyuo vifanye utaratibu kuanzisha mashamba ya kilimo biashara
Kusaya ameahidi kupatia chuo cha MATI Ukiruguru
trekta moja na kompyuta kumi (10) ili kusaidia utendaji kazi wa chuo hicho na
kuongeza kuwa kuanzia sasa watumishi wote watalipwa stahili za posho ya masaa
ya ziada toka wizarani ili kuinua ari na motisha ya kufanya kazi kwa watumishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Frenk Onesmo
alisema wanaendelea na mafunzo ya vijana katika fani za kilimo na sasa wameanza
kufundisha kilimo cha mazao kama alizeti,mdarasini na mbogamboga ili kuwajengea
uwezo.
0 comments:
Post a Comment