METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 7, 2020

SHAKA : AANIKA MAZITO KIFO CHA KARUME

Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

 Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro (CCM) kimesema genge la wapinga Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ndilo lililopanga njama hadi kumuua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume na sasa mabaki yake ndiyo yanayoendeleza chuki , hasama na ukorofi wa kisiasa nchini.

Kimefahamisha kuwa wakati tukikumbuka kifo hicho   wauaji hao  licha ya kuyapoteza maisha ya kiongozi shupavu, lakini pia Lengo ilikuwa ni kukwamisha mchakato wa malengo na sera za ASP zisifike azma ya kuleta maendeleo kusudiwa.

Msimamo huo umetolewa jana na Katibu wa CCM Shaka Hamdu Shaka ofisini kwake alipotakiwa kutoa mtazamo wake juu ya miaka 48 ya  kumbukizi ya mauaji dhidi ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Aprili 7 mwaka 1972 .

Shaka alisema hadi sasa mabaki ya wapinzani waliokizuia ASP kisishike utawala kwa njia za uchaguzi , hata pale yalipofanyika Mapinduzi, walichukizwa kuiona serikali ya wazalendo ikisimamia vyema maendeleo ya kisiasa, kujenga umoja na kukuza uchumi .

Alisema sera makini, uongozi bora, siasa safi na ustawi wa maisha ya watu ulioshamirisha maendeleo ya kisekta chini ya ASP,  hayakuwapendezesha wapinzani na kuamua kumuua kiongozi ambaye alikuwa mchapakazi, mwenye busara, dhamira na shabaha ya kuutumikia umma.

"April 7 mwaka 1972 Zanzibar ilikutwa msiba mkubwa wa kumpoteza Jemedari Hayati Mzee Abeid Karume, wapinzani wa ASP wameyakatisha maisha yake baada ya kuona akiongoza na kujenga ustawi wa maendeleo. Mabaki ya watu hao hadi sasa ndiyo wanaoeneza chokochoko , hasama na ukorofi wa kisiasa "Alisema Shaka.

Aidha Shaka alieleza kuwa vizazi vyote kikiwemo kizazi cha sasa na vijavyo, vitaendelea kusoma, kuihifadhi na kuifuatilia historia ya ASP pamoja na harakati zilizoleta ukombozi hadi kufanyika Mapinduzi na katu hakitasahau kifo cha shujaa wa huyo.

Alifahamisha kuwa ingawa miaka 48 imepita tangu Rais huyo kuuawa watanzania  wema bado wanaukukumbuka msiba wa kumpoteza Mzee Karume ambaye maisha yake yalidhulumiwa kikatili na kundi la maadui na vibaraka waliotumiwa na mabeberu .

"Tutaendelea kumkumbuka Mzee Karume milele , tunaamini kilichokufa ni kiwiliwili, fikra, malengo na shabaha za serikali ASP na TANU na sasa CCM zitadumishwa toka kizazi moja hadi kingine, kazi ya kulinda na kuisimamia misingi ya Mapinduzi itaendelezwa bila woga "Alieleza Shaka.

Shaka alikumbusha kuwa wanawatambua kwa asili na majina yao , bibi na babu zao, walioshiriki kukipinga ASP tokea mwaka 1957 kisifanikiwe kushika utawala kwa njia za uchaguzi hadi wazee walipoona ipo haja ya kuupindua utawala wa kisultan "Alisema.

Katibu huyo alisisitiza kuwa itamuenzi, kumkumbuka na kumheshimu Mzee Karume kwasababu ndiye pekee Barani Afrika aliyekuwa tayari kutekeleza dhana ya Muungano hatimaye kuafiki na kumpisha mwenzake Mwalimu Julius Nyerere awe Rais naye abaki kuwa Makamu wa Rais.

Shaka alieleza pamoja na kufanyika mikutano mingi ya Pan Afrcanism (umajumui) , iliojadili na kutolewa maazimio ya kuunda dola moja Afrika, mara baada ya nchi za kiafrika kupata uhuru , aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ndiyo waliokubali kutekeleza maazimio hayo.

"Walipokubaliana kuziunganisha nchi zao mbili huru, Mzee Karume hakutaka longolongo, alimueleza Mwalimu Nyerere, tukawaulize wananchi  wakikubali tuungane, akasema wakiafiki Rais wa Kwanza wa Muungano awe Mwalimu Nyerere, uamuzi huu viongozi wengi wa Afrika uliwashinda na bado unawatatiza "Alisisitiza Shaka

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com