METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 15, 2020

“NFRA TOENI HUDUMA, FANYENI BIASHARA, NA JIENDESHENI KWA FAIDA” – KATIBU MKUU KILIMO

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa 
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa Bwana Morgan Mwaipyana pembeni yake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo, Bi. Hilda Kinanga
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa Bwana Morgan Mwaipyana pembeni yake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo, Bi. Hilda Kinanga mbele ni sehemu ya Watumishi wa NFRA Kanda ya Kipawa
Watumishi wa NFRA Kanda ya Kipawa wakimsiliza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Watumishi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa 

Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bwana Gerald Musabila Kusaya amewataka Watumishi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa kufanya kazi kwa ubunifu ili kuifanya Taasisi hiyo ijiendeshe kwa tija na ufanisi mkubwa.

Katibu Mkuu, ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembela Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha, kujifunza namna Watumishi wa Taasisi hizo wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na Watumishi wa NFRA Kanda ya Kipawa, Bwana Gerald Kusaya, kwanza amewapongeza Watumishi wote kwa namna wanavyojitoa katika kutekeleza majukumu yao lakini pia amewataka kuwapa ushirikiano Viongozi wao na kuendelea kufanya kazi kama timu na familia moja.

“Fanyeni kazi kama timu, hiyo ndiyo siri ya mafanikio lakini pia napenda mfahamu kuwa Mimi kama Kiongozi wenu; nipo na ninawaunga mkono”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa Taasisi ya NFRA Kanda ya Kipawa ina jukumu kubwa la kuhifadhi chakula kwa ajili ya kuhudumia mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara na kuongeza kuwa licha ya kutoa huduma kwa Watanzania lakini kuna haja ya kuongeza ubunifu kwa kujiendesha kibiashara.

“Nafahamu, mnatoa huduma kwa Watanzania, lakini Mimi kama Katibu Mkuu wenu; nawashauri mtoe huduma lakini pia fanyeni biashara na mwisho wa siku msipate hasara”.

“NFRA ni Taasisi inayofahamika, nendeni Benki ili mkope fedha kwa ajili ajili ya kuendesha miradi mikubwa ya biashara na siku hizi tuna benki maalum inayohudumia Sekta ya Kilimo Mazao, Benki ya Kilimo (TADB) itumieni, na binafsi nipo kama mtapata changamoto yoyote; njooni hata bila mihadi (Appointment) na nitawaunga mkono.” Amekaririwa Katibu Mkuu.

Wakati huohuo Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amewahakikishi Watanzania kuwa Taifa lina akiba ya kutosha ya chakula na kwamba licha ya changamoto ya ugonjwa wa homa ya mapafu, unaosababishwa na kirusi ina ya “Corona” akiba ya chakula ya taifa, ina chakula cha kutosha.

“Niwahakikishie Watanzania wenzangu kuwa Taifa letu lina chakula cha kutosha na kuna maeneo yanauzalishaji mzuri kwa kuwa yalipata mvua za vuli na yanaendelea kupata mvua za masika vizuri”. Amemalizia Katibu Mkuu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com