METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 15, 2020

KATIBU MKUU KILIMO AIAGIZA BODI NA MENEJIMENTI YA MAMLAKA YA UDHIBITI WA MBOLEA (TFRA) KUJA NA MKAKATI WA NAMNA YA KUVUTIA UWEKEZAJI ZAIDI WA VIWANDA VYA MBOLEA HAPA NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Musabila Kusaya akizungumza na vyombo vya habari ofisi kwake, Jengo la Kilimo I, Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam

Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bwana Gerald Musabila Kusaya, ameiagiza Bodi na Menejiment ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea, kuandaa mkakati wa uanzishwaji wa viwanda vipya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa pembejeo hiyo hapa hapa nchini.

Katibu Mkuu, amesema Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea, ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa uzalishaji wa ndani wa mbolea, unapewa kipaumbele na kwa kuongeza uanzishwaji wa viwanda vipya; mbolea itakuwa ikipatikana kwa urahisi, nafuu na kila Mkulima atamudu kuinunua na kuitumia.

“Nimeelezwa hapo awali kuwa, nchini tuna viwanda 11 vinavyotengeneza mbolea lakini ukiangalia, vinazalisha asilimia 10 tu ya mahitaji yetu ya ndani, tunawajiba kuongeza ubunifu ili kujenga mazingira mazuri kwa Wageni na Watanzania kujenga viwanda hapa hapa nchini”

“Tukijenga mazingira mazuri ya Wazawa na Wageni kujenga viwanda vipya hapa hapa nchini, mbolea haitauzwa kwa bei ya shilingi 53,000 na kwa mfuko wa kilogramu 50, ambapo ni Wakulima wachache wanaoweza kumudu bei hii.” Amekaririwa Katibu Mkuu.

Bwana Gerald Kusaya ameongeza kuwa Bodi na Menejimenti ya TFRA ibuni mkakati wa namna bora ya kuongeza uwekezaji hapa hapa nchini, kwa kuwa hilo ndiyo suluhisho la kweli katika kuwahakikishia Wakulima wengi wadogo unafuu bei.

Aidha Katibu Mkuu, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Dkt. Stephan Ngailo kuandaa ziara fupi ambapo, yeye (Katibu Mkuu), Bodi na Menejimenti ya TFRA itatembelea viwanda kadhaa vya ndani kwa lengo la kuwasikiliza Wamiliki wa viwanda hivyo, changamoto wanazokutana pamoja na kukwamua kama kuna vizuizi wanavyokutana navyo katika uendeshaji wa biashara ya mbolea.

Katibu Mkuu amewataka Watumishi wa TFRA kuongeza udhibiti kwenye usimamizi wa ubora wa mbolea hususan kwenye mikoa yenye matumizi makubwa ya mbolea.

“Niwaome muendelee kufanya kazi kwa bidii lakini pia muongeze udhibiti kwa kushirikiana na Serikali za mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi ili kuhakikisha mbolea inafika kwa wakati lakini pia isitoloshwe kwa njia haramu”. Amesisitiza Katibu Mkuu.

Aidha Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amesema anavutiwa na utendaji kazi wa Watumishi wa TFRA ambapo ameahidi kutoa pikipiki tano (5) ambazo Wizara inataraji kupokea vitendea kazi kadhaa yakiwemo magari na pikipiki kutoka kwenye Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa zao la Mpunga (ERPP), Mradi ambao unataraji kumalizika hivi karibuni. Pikipiki hizo watapewa Wakaguzi wa Mbolea katika Kanda ambazo TFRA inatekeleza majukumu yake.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com