Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akingea na watumishi wa Bodi ya Pamba nchini ambapo amewataka kubuni mikakati mipya ya kuongeza uzalishaji wa pamba nchini ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya kuongeza thamani ya zao hilo.Tukio hili limefanyika leo jijini Mwanza
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (aliyevaa tai) akiongea na Menejiment ya Chama Kikuu cha Ushirika Mwanza (Nyanza) na kuwataka kujitegemea kimapato kwa kutumia rasilimali za wakulima zilizopo.Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Nyanza Benjamin Mikomangwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akizungumza na watumishi wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) ambapo amekitaka chama kikuu hicho kuhakikisha kinarejesha mali zote zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha utaratibu kama nyumba na mashamba.
Wizara ya Kilimo imekiagiza Chama Kikuu cha
Ushirika mkoani Mwanza (Nyanza) kubuni njia muafaka za kujitegemea kiundeshaji
kwa kutumia rasilimali nyingi ilizonazo.
Agizo hilo limetolewa leo(30.04.2020) Jijini
Mwanza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofanya kikao na
watumishi wa chama hicho na kuelezea kusikitishwa kwake na hali ya utendaji wa
chama hicho kushindwa kujiendesha.
“ Tunataka kuona sasa Nyanza mnakuwa na
utendaji unaolenga kujiendesha kibiashara tofauti na ilivyokuwa zamani ili
wakulima wa pamba wanufaike na ushirika
kupitia mali zao” alisema Kusaya
Alibainisha kuwa wizara ya Kilimo ina lengo la
kuiona Nyanza inasimama yenyewe na ya kisasa inayojiendesha kibiashara
kuwakomboa wakulima wa pamba.
Kusaya alisema Chama Kikuu cha Nyanza kinazo
mali nyingi ikiwemo nyumba,maghala na mashamba ambayo kwa sasa hazitumiki
kuzalisha mali kwa faida na kuwa zingine bado zinamilikwa isivyo halali na
baadhi ya watu na kutaka ripoti ya mali hizo ipelekwe wizarani kwake ifikiapo
Mei 15 mwaka huu.
“ Watieni moyo wana ushirika ili wawe na imani
na Nyanza.Nataka nione mkijitegemea na kuwa leo nilitegemea kusika ripoti ya
mafanikio badala ya kunieleza matatizo ya madeni” alisema
Aidha aliagiza kuwa agizo la Waziria Mkuu
kuhusu urejeshwaji wa nyumba nane (8) zilizokuwa zikimilikiwa isivyo na watu
binafsi litekelezwa kwa nyumba hizo kuwa na hati miliki za umma .
Kwa uande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Nyanza Martha
Ndeto alisema tayari nyumba saba(7) zilizokuwa zikimilikiwa kinyume ya
utaratibu zimerejeshwa na hati zake zipo kwa Msajili wa Ardhi na kuwa kazi
inaendelea kufuatilia moja iliyobaki.
Ndeto aliongeza kusema Nyanza kwa sasa
inakabiliwa na madeni makubwa yanayofikia shilingi Bilioni 4.23 toka wa
mabenki,taasisi za serikali na wafanyabiashara.
Katika hatua nyingine Katibu mkuu Kusaya
alitembelea Bodi ya Pamba yenye makao makuu yake jijini Mwanza na kuagiza kuwa
waongeze malengo ya uzalishaji pamba kutoka tani 450,000 za sasa hadi tani
700,000 mwaka ujao .
Alisema amesikitishwa kuona viwanda vya
kuchambua pamba kwenye mikoa ya Shinyanga,Simiyu na Mwanza vinashindwa kufanya
kazi mwaka mzima kutokana na upungufu wa malighafi.
“ Nia yangu nikiwa Mtendaji Mkuu wa Wizara ya
Kilimo ni kuona uzalishaji wa pamba unaongezeka ili viwanda vipate malighafi ya
kutosha na wakulima wapate fedha za kutosha “ alisisitiza Katibu Mkuu huyo
Mkurugezi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco
Mtunga alisema bodi yake inaendelea na mikakati ya kuongeza uzalishaji pamba na
kukutafuta pembejeo za kutosha ili
wakulima wapate mavuno bora mengi na soko la uhakika.
Katibu Mkuu Kusaya yupo katika ziara ya kikazi
mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua maandalizi ya msimu wa ununuzi wa pamba utakaonza
hivi karibuni na kuongeza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara yake.
0 comments:
Post a Comment