Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa barabara ya muda katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa, Machi 10, 2020. Wa tatu kushoto ni mkewe, Mary na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Rota Sanare. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patric Mfugale (mwenye kofia) wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya muda katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa Machi 10, 2020. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Kazi ya ujenzi wa barabara ya muda katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa Machi 10, 2020. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi huo leo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa barabara ya muda kwenye eneo la daraja la Kiyegeya na kusema kazi inaenda vizuri sababu hakuna tena msongamano wa magari kama ilivyokuwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa yote nchini wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote siyo kwa juu tu bali hadi chini ya madaraja ili kujiridhisha na usalama wake.
“Nilitoa agizo kwa mameneja wa TANROADS ambao wana highways, wazikague kila mara kwa sababu hatuhitaji kuwa na highways zilizobomoka.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Machi 10, 2020) wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, mara baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ujenzi wa barabara ya muda ili kurejesha mawasiliano na mikoa mingine.
“Nimekuja kuona kazi inaendeleaje, nimekuta msongamano wa magari hakuna kama ilivyokuwa wiki iliyopita. Ile diversion (barabara ya mchepuko) imesaidia kuondoa msongano uliokuwepo,” amesema Waziri Mkuu.
“Mahitaji yetu ni kuwa na daraja la kudumu, kwa hiyo mharakishe ujenzi wa daraja hilo, Mmesema sasa hivi mnapanga kuweka daraja la zege ili maji yakija kwa wingi yaweze kupita juu ya hii barabara ya muda, msisitizo ni kukamilisha kazi ya daraja la kudumu,” amesema wakati akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale.
Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu alibaini kuwa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.
“Uamuzi niliochukua wa kumhamisha Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ulikuwa sahihi kwa sababu huyu Bwana anaonekana hawezi kazi ya kusimamia wengine. Fedha ya ukaguzi ipo, ya ujenzi ipo, halafu kazi haifanyiki. Kazi ya kusupervise haiwezi, kwa hiyo, ateuliwe Meneja mwingine,” alisisitiza.
“Nilimuuliza meneja aliyekuwepo kama wana fedha za ukaguzi, akasema anayo. Nikamuuliza kama anayo fedha ya spot maintenance, akasema anayo. Fedha hizi zote zilipaswa zitumike kwa kazi iliyopangwa, lakini hilo halikufanyika.”
Akijibu hoja hiyo, Mhandishi Mfugale alisema amemuacha Mhandisi Godwin Andalwisye aendelee kuwepo pale site kwa sababu ya utalaamu wake kweye madaraja. “Ulishatoa maelekezo kuwa aondolewe, na wa kumhamisha ni mimi, tunatumia tu utaalmu wake.
Alipoulizwa kama ameshateua Meneja mwingine wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mfugale alikiri kwamba bado hajamteua mtu mwingine.
Jumatano iliyopita, (Machi 4, 2020) Waziri Mkuu alikatisha ziara yake mkoani Tanga na kutembelea eneo hilo ambako alishuhudia mlundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.
Aliagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja kwa sababu ya kuzembea kutimiza wajibu wake.
Waziri Mkuu ambaye alisafiri kwa magari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, pia alisimama Morogoro na kukagua ujenzi wa uzio wa makaburi ya Kola Hill ambako walizikwa wahanga wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kulipuka Agosti 10, 2019 na kuua watu 115, kati yao wanaume walikuwa ni 109 na wanawake ni sita.
Akiwa makaburini hapo, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Morogoro uweke utaratibu wa kuwa na mtu maalum atakayesimamia masuala ya mazishi yote yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kola Hill.
Amesema mtu huyo ahakikishe makaburi yote yanachimbwa katika utaratibu na mpangilio utakaoliwezesha eneo hilo kuwa na nafasi ya kuzika watu wengi. “Utaratibu wa sasa wa kuchimba makaburi kiholela utalifanya eneo hili lijae haraka huku likiwa halina mpangilio maalum.”
Waziri Mkuu pia aliridhia maombi ya uongozi wa mkoa wa Morogoro ya kutaka akubali makaburi hayo yajengewe ili yawe na muonekano mzuri kazi ambayo itagharimu zaidi ya sh. milioni 12.
Uongozi huo pia uliomba rdhaa ya Waziri Mkuu kutengeneza mandhari ya ndani ya uzio (Landscaping) kazi ambayo itagharimu sh. 1,682,500/- pamoja na kujenga mnara wa kumbukumbu kwa gharama ya sh. 4,173,125/-.
0 comments:
Post a Comment