Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akisalimiana kwa mtindo wa kugonganisha miguu na mmoja wa wakazi wa kijiji cha Farkwa wilayani Chemba alipofika katika kijiji hicho kuwasha umeme na kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme katika wilaya hiyo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga( katikati)wakiteta jambo wakati Dkt. Kalemani alipofika katika wilaya hiyo kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mameneja wa TANESCO na REA kusimamia uondoaji wa nguzo za umeme zilizolazwa chini katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Chemba.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa onyo na kupiga marufuku wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini nchi nzima, kulaza nguzo za umeme chini kwa muda mrefu,badala yake ndani ya siku tatu nguzo hizo ziwe zimefikishwa eneo la mradi na kusimikwa.
Pia alitoa muda wa siku tatu kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa REA mkoani Dodoma kuondoa nguzo zote ambazo zimelazwa chini katika Mkoa huo na kuzisimika katika maeneo husika, kinyume cha hapo mhandisi na mkandarasi watachukuliwa hatua.
Dkt. Kalemani alitoa onyo hilo, Machi 4, 2020, wakati wa kuwasha umeme katika kijiji cha Farkwa kilichopo wilayani Chemba mkoani Dodoma.
Alisema kumekuwa na tabia ya wakandarasi kuacha nguzo zikiwa chini kwa muda mrefu bila kusimikwa jambo ambalo limesababisha baadhi ya nguzo kuharibika na fedha za serikali kupotea.
Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka Wakurugenzi wa Tanesco na Mkurugenzi wa REA kuhakikisha wanasimamia maagizo hayo kwa ukaribu na umakini.
“Hili ni onyo la mwisho, nimepita barabarani nimekuta nguzo zimelala, sasa Meneja wa TANESCO Kanda na Mikoa simamieni maelekezo haya nguzo zote zilizolazwa chini kwenye mikoa nchi mzima ziondolewe na zikajengwe”, alisema Dkt. Kalemani.
“Nasema siku tatu kutoka leo, Machi 4, 2020, nguzo zilizolazwa chini mkoani Dodoma ziondolewe, tofauti na hivyo mhandisi achia ngazi, mkandarasi utaandikiwa barua ya kufuta mkataba wako, nakueleza mapema tena hadharani! meneja lisimamie hili”, alisisitiza Dkt.Kalemani. Alisema serikali imetoa Shilingi bilioni 40.2 kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini.
Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali inavitu vingi vya kuwahudumia wananchi kama sekta ya maji, afya, barabara na elimu lakini bado imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha vijiji vyote vinapatiwa umeme.
Alisema pamoja na juhudi za serikali za kupeleka umeme maeneo mengi, lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya maeneo ambayo hayajafikiwa na kuwa serikali inafanya kila liwezekanalo kuiangaza Tanzania yote.
“Na hili ni onyo kwa wakandarasi wote nchi nzima ni marufuku kuanzia sasa nguzo kulazwa chini kwa muda mrefu, zikifika ndani ya siku tatu zikasimikwe na zikajengwe ili wananchi wakapate umeme.”
Akizungumzia uwashaji wa umeme katika kijiji cha Farkwa, Dkt. Kalemani alisema uwashwaji wa umeme katika kijiji hicho unaifanya idadi ya vijiji vya Wilaya ya Chemba vilivyofikiwa nishati ya umeme kufikia 85 kati ya vijiji 114, na kuwahidi wananchi wa eneo hilo kuwa vijiji vyote vilivyosalia pia vitafikiwa na umeme ndani ya muda uliopangwa.
Aidha, Dkt.Kalemani aliwaagiza Mameneja wa REA na TANESCO kuhakikisha vijiji vilivyobaki katika kata ya Farkwa kufikishiwa nishati hiyo ndani ya miezi miwili ijayo na kumuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga kusimamia hilo.
Pia alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kutumia umeme huo kwa kuanzisha shughuli za kiuchumi ikiwamo uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na kuwa hiyo itakuwa ni kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Haiwezekani serikali ikatoa fedha ya kuwafikishia wananchi umeme tena kwa gharama nafuu, halafu wewe mwananchi usiutumie, tutapita kila kaya kukagua na tukikuta hujaweka umeme tutapiga mnada na kuuza kuku au mbuzi na kukuwekea umeme kwa lazima,hivyo hakikisheni najiunganishia nishati hiyo”, alisema Dkt. Kalemani Pia aliwasihi wananchi wa Farkwa na maeneo mengine kuhakikisha wanatunza miundombinu ya umeme ili iweze kuwasaidia wananchi.
Naye Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia pamoja na kuipongeza serikali kwa kazi ya kuwafikishia wananchi nishati hiyo aliomba maeneo ambayo bado hajafikiwa yafikiwe ili wananchi waweze kujiletea maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Saimon Odunga aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishwa umeme kwa Shilingi 27,000 kupata huduma hiyo wakati mradi unaendelea.
0 comments:
Post a Comment