METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, February 20, 2020

ZUNGU ATOA ONYO KALI KWA WANAOKIKA SHERIA NA KUTOA MAELEKEZO KWA NEMC

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akiongea na wadau katika kikao cha kukuza uelewa wa Sheria na Utekelezaji wa Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki kwa Wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa Mifuko mbadala ya Plastiki. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa LAPF, Jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha (kushoto) Ni Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka, Bi. Kemilembe Mutasa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira na Bw. Jabir Abdi Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Viwango Tanzania.
Bw. Mushtak Waliji Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Plastiki nchini akichangia mada katika kikao cha kukuza uelewa wa Sheria na Utekelezaji wa Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki kwa Wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa Mifuko mbadala ya Plastiki. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa LAPF, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu hii leo ametembelea eneo la Karakata Mji mpya kujionea changamoto za Mto Msimbazi, katika ziara hiyo ameambatana na Mbunge wa Segerea Mhe. Bona Kamoli.
Picha ikionyesha mmomonyoko wa ardhi eneo la Karakata ambao Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ameelekeza wataalamu wa NEMC na Jiji la Dar es Salaam kushirikiana na kupata ufumbuzi wa haraka.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Zungu amesema katika kipindi hiki cha miezi tisa (9) tangu Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Kupiga marufuku mifuko ya Plastiki za mwaka 2019 zianze kutekelezwa, Serikali imefanya jitihada za kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, kuandaa viwango vya ubora wa mifuko mbadala ya Non-woven, kufanya kaguzi katika maeneo ya uzalishaji, usambaji na uuzaji wa mifuko mbadala.

Akifungua kikao cha wadau katika ukumbi wa LAPF, Kijitonyama chenye lengo la kukuza uelewa wa Sheria na Utekelezaji wa Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki kwa wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa mifuko mbadala Jijjini Dar es Salaam, Zungu ameainisha kuwa mifuko mbadala inayoruhusiwa kisheria kutumika kubebea bidhaa hapa nchini ni lazima ikidhi matakwa ya kisheria.

“Mwongozo umeainisha viwango vya ubora wa mifuko mbadala ya “Non-woven” ni uzito usiopungua 70GSM; iwe inayoweza kurejelezwa (recyclable); iwe na anuani ya mzalishaji au nembo ya biashara (trade mark); ionyeshe uwezo wake wa kubeba (carrying capacity); na iwe imethibitishwa ubora wake na Shirika la Viwango-TBS” Zungu alisisitiza.

Waziri Zungu amesema kuwa hadi sasa tani 54 za mifuko aina ya non-Woven zimekamatwa na kusisitiza kuwa hivi sasa adhabu kali zitatolewa ikiwa ni pamoja na faini, kufunga viwanda na kusisitiza kuwa msako mkali unaanza kwa wazalishaji na wasambazaji wa mifuko isiyokidhi viwango.

“Katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Juni, mosi 2019 shehena ya mifuko mbadala isiyokidhi viwango isiyopungua tani 54.035, katoni 12,767 na vipisi 11,191, 919 imekamatwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara wakati wa kaguzi na hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake, zimechukuliwa kwa waliokutwa na makosa. Hatutishani lakini tunatoa tahadhari! Wenye viwanda wanaoendelea kukaidi wakikamatwa watashtakiwa kwa kuhujumu uchumi” Zungu alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Zungu amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) kuitisha kikao cha wakurugenzi na Wataalamu wa Mazingira katika Halmashauri zote nchini kuwakumbusha majukumu yao ya kusimamia ipasavyo katazo la Mifuko ya Plastiki na kuendelea na utoaji wa elimu kwa umma.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hiifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini Dk. Samuel Gwamaka amesema Serikali imefanikiwa kusimamia katazo la Mifuko ya Plastiki ingawa kuna changamoto ambazo Ofisi yake inazifanyia kazi kwa karibu.

Amesema kuwa changamoto kubwa ni kutojitangaza kwa wafanyabiashara wa mifuko
mbadala kwa kutumia vyombo vya habari.

“Inakuwa vita hivi tunapiga sisi wenyewe, tunaowapigania wao wamekaa pembeni, natoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu, tunalinda mazingira kwa vizazi vijavyo, suala

hili linahitaji elimu endelevu na sisi tutaendelea kufanya hivyo” amesisitiza Dkt. Gwamaka.
Dkt. Gwamaka amelipongeza Jeshi la polisi Makao Makuu (Kitengo cha Mazingira) kwa mchango mkubwa wanaotoa kwa Baraza ikiwa ni pamoja na kusimamia kikamilifu Katazo la Mifuko ya Plastiki.

Dkt Gwamaka amesema kuwa mpaka sasa Viwanda 72 vya kuzalisha mifuko mbadala vinafanya kazi hapa nchini na kutoa ajira takriban 2761. Kikao cha kukuza uelewa wa Sheria na Utekelezaji wa Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki kwa Wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa Mifuko mbadala ya Plastiki kimefanyika katika Ukumbi wa LAPF, Jijini Dar es Salaam.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com