Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Mohamed Utaly akiongea na watumishi
wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa
Baraza la wafanyakazi wa Mfuko huo
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard
Konga akiongea na watumishi wa mfuko huo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa
Baraza la wafanyakazi
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la NHIF wakiwa wameshikana mikono kama
ishara ya mshikamano wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la nne.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia mada za mkutano
KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Mohamed Utaly amewatakaWatumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwa wazalendo, waadilifu na kufanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha Mfuko unabaki na uhai wake na unahudumia vizazi na vizazi.
Amesema kuwa kutokana na Mfuko kwa sasa kuwa nyenzo na nguzo muhimu katika Sekta ya afya hakuna namna ambayo mwananchi yoyote anaweza kuwa na amani bila kuwa na bima ya afya ambayo inamuwezesha kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote.
Bw. Utaly ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa nne wa Baraza la Wafanyakazi la NHIF mjini Morogoro ambapo aliutaka Mfuko kuhakikisha unaendelea na mikakati ya kuwafikia wananchi katika maeneo yao ili wawaelimishe na kuwahamasisha kujiunga na bima ya afya.
“Jambo muhimu ambalo mnatakiwa kuzingatia ni kwamba Serikali ya Awamu ya tano imedhamiria kumpa kila mtanzania maisha bora. Hivyo Mfuko unatakiwa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora kwa kuhakikisha wanajiunga na bima ya afya na wanapata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima,” alisema Bw. Utaly.
Alisema kuwa kwa sasa wananchi wameelewa dhana ya bima ya afya ikilinganishwa na hapo awali wakati NHIF inaanzishwa ambapo kulikuwa na upinzani mkubwa ndani ya jamii hususan kwa vyama vya wafanyakazi hivyo kazi kubwa iliyopo katika Mfuko ni Watumishi kuendelea na mikakati ya kuwafikia wananchi.
“Mfuko huu una historia kubwa, mimi nilikuwepo wakati mjadala wa uanzishwaji wake unapita katika vyama vya wafanyakazi, ni kazi kubwa iliyofanyika mpaka hapa, watumishi wa umma ndio walikuwa mstari wa mbele kupinga lakini kwa nyakati hizi watumishi hawa hawa ndio watetezi wa huduma za Mfuko huu kutokana na umuhimu wake katika maisha ya kila siku,” alisema Bw. Utaly.
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Bw. Bernard Konga alisema kuwa kikao hicho kina agenda za kuweka mipango thabiti ya uboreshaji wa huduma katika maeneo yote kupitia mipango ya mwaka wa fedha 2020/2021 na mpango mkakati wa miaka mitano ijayo.
Alisema kuwa Mfuko umetekeleza maagizo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuanzisha mpango unaowawezesha kila mwananchi kujiunga na huduma za bima ya afya.
“Katika hili tumejipanga katika maeneo yote yakiwemo ya huduma kwa wanachama wetu, kwa sasa tunaendelea na kampeni mbalimbali za uhamasishaji
wananchi katika maeneo yote ili wananchi wengi zaidi waweze kuwa ndani ya utaratibu wa bima ya afya,” alisema Bw. Konga.
Kutokana na hayo, ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua haraka za kujiunga na NHIF kupitia mpango wa vifurushi ambavyo vimezingatia hali halisi ya mahitaji ya huduma na uwezo wa wananchi katika kuchagia huduma hizo.
0 comments:
Post a Comment