MKUU, Kassim Majaliwa amesema juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji wa kodi zimewezesha mapato ya kodi kwa Desemba, 2019 kuvunja rekodi na kufikia sh. trilioni 1.92.
Amesema hatua hiyo inatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na RaisDkt. John Pombe Magufuli, baada yakuongezeka kwa uzalishaji katika sekta rasmi na isiyo rasmi, ambazo zimewezesha Serikali kukusanya mapato zaidi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 7,2020) wakati akiahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 bungeni jijini Dodoma. Amesema juhudi hizo zimedhihirika wazi katika nyanja za kiuchumi na kijamii baada ya viashiria vingi vya kiuchumi vinaonesha matokeo mazuri.
Waziri Mkuu amesema mfano, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, mapato ya kodi yaliongezeka hadi kufikia wastani wa sh. trilioni 1.52 kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa sh. trilioni 1.30 katika kipindi kama hicho mwaka 2018
“Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2019, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 6.8. Aidha, ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika robo ya tatu ya mwaka 2019 ulikua kwa viwango vifuatavyo: Kenya (asilimia 5.1); Uganda (asilimia 2.7); na Rwanda (asilimia 11.9).”
Amesema ukuaji huo wa uchumi, umechangia kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta rasmi na isiyo rasmi pamoja na mambo mengine, juhudi za Serikali zimesaidia kuimarisha uwekezaji katika miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, reli, na viwanja vya ndege na kutengemaa kwa upatikanaji wa huduma za maji.
Pamoja na kuimarika kwa huduma za usafirishaji; habari na mawasiliano; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kumekuwa chachu ya mafanikio hayo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu matumizi katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, ambapo amesema Serikali imetumia sh. trilioni 15.32, sawa na asilimia 91.2 ya lengo.
Amesema fedha hizo zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ulipaji wa mishahara ya watumishi, ugharamiaji wa deni la Serikali.
Kugharamia ulipaji wa madai ya ndani yaliyohakikiwa (watumishi, wazabuni na wakandarasi) na uendeshaji wa shughuli za Serikali katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
0 comments:
Post a Comment