Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na watumishi wa ofisini kwake (hawapo pichani) pembeni yake ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Benard Makali.
********************************
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo juu ya kutojihusisha na siasa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais na kuwataka kutunza siri za serikali na kuachana na kawaida ya kupiga picha nyaraka za serikali na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii hali inayokiuka maadili ya utumishi wa umma.
Amesema kuwa kuna tabia ya watumishi wa ofisi hiyo kujihusisha na kuwa mawakala wa wanasiasa na kutahadharisha kutotumia vibaya nafasi walizonazo na kwaajili hiyo wajiwekeze kwenye kuendeleza shughuli za kimaendeleo za mkoa kwani endapo nafasi hiyo itawatoka hawatakuwa na namna zaidi ya kuhangaika kutafuta ajira katika taasisi zisizo za kiserikali ambazo upatikanaji wake sio rahisi.
“Kipindi hiki ni cha pirika pirika nyingi za kisiasa na wengine wanapenda kufanya siasa tukumbuke kwamba sisi ni watumishi wa serikali hatupaswi kufanya siasa kazini lakini pia ni lazima tutunze siri za ofisini kwetu, tusitumike, watumishi wa Regional Secretariat wasijihusishe kuwa mawakala wa wanasiasa, imetokea mara kadhaa tunaona mtu anaipiga picha barua ya serikali halafu kwenye mtandao, watumishi tutunze siri za ofisi,” alisisitiza.
Aidha, amewataka watumishi hao kupunguza matumizi ya simu wakati wa kazi na kumuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha huduma ya mtandao inayopatikana katika ofisi hiyo inatumika kwaajili ya shughuli za ofisi na kuongeza kuwa watumishi hao bado wanahitaji kufundishwa namna ya kuongea vizuri na wateja wanaofika kupata huduma katika ofisi hizo.
Halikadhalika, Mh. Wangabo amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha anaweka utaratibu maalum kwaajili ya kulipa maadeni yanayodaiwa na watumishi hao ili kuleta ufanisi wa kazi katika ofisi, na kuwataka watumishi hao kujitathmini katika uwajibikaji na uchapakazi, na kuwa na tabia ya kutunza vifaa vya ofisi ili kutumia fedha nyingine katika maendeleo.
Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati alipofanya kikao na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa juu ya tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka 2019 pamoja na kuwashukuru kwa ushirikiano wao katika wa kazi pamoja na uchache wao jambo ambalo serikali inalifanyia kazi ili kuongeza watumishi.
0 comments:
Post a Comment