Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akitoa
taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu
mwaka wa fedha 2019/2020. Kulia kwake ni
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kushoto kwake ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara
ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini wakiwa katika kikao na Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilicholenga
kujadili kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha za miradi ya umeme vijijini katika kipindi cha nusu
mwaka wa fedha 2019/2020.
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake
wakiwa katika kikao na Wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani) kilichohusu hali ya
upatikanaji wa fedha za miradi ya umeme
vijijini katika kipindi cha nusu mwaka
wa fedha 2019/2020.
Imeelezwa kuwa, Mradi wa usambazaji umeme vijijini
wa Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili,
(Turnkey Phase III-Round II) utaanza kutekelezwa mwezi Februari, 2020 ambao utakamilisha
lengo la Serikali la kupeleka umeme katika vijiji 12,268 ifikapo mwaka 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani alisema
hayo wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu hali ya
upatikanaji wa fedha za miradi ya umeme
vijijini katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020.
Katika kikao hicho aliambatana na Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard
Masanja, Menejimenti ya Wizara pamoja
Wenyeviti wa Bodi na Menejimenti za Taasisi zilizo chini ya Wizara.
Dkt.Kalemani alisema kuwa, mradi huo
utasambaza umeme katika vijiji 1,822 ambavyo havikuwepo katika mradi usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu
mzunguko wa kwanza ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.
Akitoa takwimu za usambazaji umeme vijijini, Dkt
Kalemani alisema kuwa hadi kufikia mwezi Disemba 2015, jumla ya vijiji 2,018
vilikuwa na umeme na hadi kufikia Januari 10, 2020 jumla ya vijiji 8,408 vimepatiwa umeme ambayo ni sawa na
asilimia 69.
Vilevile, alisema kuwa kutokana na miradi
mbalimbali ya usambazaji umeme vijijini inayoendelea, inatarajiwa kuwa, kufikia
mwezi Juni mwaka 2020, jumla ya vijiji 10,446 vitakuwa vimesambaziwa umeme.
Aidha, kuhusu wakandarasi wanaosuasua katika
utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, alisema kuwa, tayari wameshaandikiwa
barua za kusudio la kusitisha mkataba na kampuni hizo zimepewa siku 60 za kurekebisha
mapungufu la sivyo hatua zaidi za kimkataba zitachukuliwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala
wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, aliieleza Kamati hiyo kuhusu
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme vijijini ukiwemo wa kusambaza nishati
jadidifu katika maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa pamoja na visiwa.
Kuhusu mradi huo, alisema kuwa, Serikali kupitia
Mfuko wa Nishati Vijijini kwa kushirikiana na Serikali za Sweden na Uingereza
umetoa ruzuku kwa kampuni binafsi 14 ili kuvipatia umeme vijiji 119 kutokana na
vyanzo vya nishati jadidifu ambapo vijiji 95 vimepelekewa umeme.
Kuhusu kupeleka umeme visiwani, Maganga alisema
kuwa, jumla ya visiwa 22 kati ya 196 vimesambaziwa umeme kupitia mradi wa
usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu na kwamba visiwa vyote vitasambaziwa umeme
ifikapo mwaka 2021.
Aidha, kuhusu suala la usambazaji umeme kwenye
Taasisi za umma, alisema kuwa, hadi kufikia Disemba 2015 jumla ya Taasisi 4,036
ziliunganishiwa umeme na hadi kufikia Disemba 2019 jumla ya taasisi 11,070
zimesambaziwa umeme.
Katika kikao hicho, Kamati ya Bunge iliipongeza
Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
umeme ukiwemo wa Julius Nyerere (MW 2115), aidha Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa
maoni mbalimbali yatakayoboresha Sekta ya Nishati nchini.
0 comments:
Post a Comment