Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewataka wajumbe kutoa ushauri na mawazo yenye tija kuhusu Mpango na Bajeti hiyo kwa lengo la kuboresha huduma kwa Jamii na kukamilisha miradi ya maendeleo ambayo manispaa imeanzisha
NA FREDY MGUNDA, IRINGA
WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri ya Manispaa ya Iringa (DCC) wamepitisha makisio ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya shilingi bilioni 35 kwa ajili ya mwaka wa fedha ujao wa fedha wa 2020/2021.
Wajumbe hao walipitisha mapendekezo hayo jana baada ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya ya Iringa, Omary Mshangama kuwasilisha wakati wa kikao kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2020/21.
Akifungua Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki, Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewataka wajumbe kutoa ushauri na mawazo yenye tija kuhusu Mpango na Bajeti hiyo kwa lengo la kuboresha huduma kwa Jamii na kukamilisha miradi ya maendeleo ambayo manispaa imeanzisha.
Kasesela akichangia kwenye kikao hicho alipendekeza kuwepo na barabara kiwango cha lami kutoka Mkwawa kuelekea Darajani kwenye barabara inayoelekea Pawaga yenye km 7 kwa kuwa ndio mfumuko mpya wa manispaa ya Iringa kuelekea kuwa jiji.
Alipendekeza kuomba serikali katika mipango ya miaka 5 hadi kumi kuuunganishwa kwa reli ili iweze kufika kwa kuwa itarahisisha usafiri kwa wananchi na kuongeza utalii kwa mkoa wa Iringa na uwezekano wa kutengeneza km 250 kwa serikali ya awamu ya tano ni rahisi kiasi cha kuweka mipango na kufikisha kwenye kikao cha ushauri mkoa wa Iringa(RCC).
Aidha Kasesela alipendekeza kuajiliwa kwa watendaji wa mitaa kutokana na upungufu uliopo hivyo ipo haja kwa mkurugenzi wa manispaa kufatilia maombi ya kuwaajili watendaji hao ili kila mtaa katika kuelekea kwenye uchaguzi kuwe na watendaji.
Alipendekeza kwenye kikao hicho kwa halmashauri kununua magari mapya ya taka na kuwapongeza kwa manispaa kujiongeza katika kuzalisha matofali ambayo kwa kiasi kikubwa kimepunguza gharama katika ujenzi wa miradi ya maendeleo na kuzishauri halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Iringa, Omary Mshangama alisema kuwa halmashauri ina kasimia na kukusanya kiasi cha sh. Bilioni 35.3 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utoaji huduma.
Alisema kuwa kati ya fedha hizo sh. Bilioni 24.09 kwa ajili ya ulipaji wa mishahara, sh bilioni 5.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo za bajeti bilioni 5.2 ni makusanyo ya ndani halisi na mapato ya uchangiaji huduma.
Mshangama alisema kuwa milioni 910.4 ni ruzuku kwa ajili ya matumizi mengineyo wakati kati ya hizo milioni 124.5 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika bajeti ya mengineyo.
Alivitaja vipaumbele vya bajeti ijayo kuwa ni ujenzi wa soko la Kihesa, ujenzi wa jengo la ofisi kuu ya ghorofa moja, kuimarisha shughuli za usafiri ambapo manispaa imepanga kununua gari moja pamoja na kukarabati magari manne.
Aidha alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuwajengea uwezo wananchi kiuchumi kwa kuimarisha mfuko wa vijana, wanawake na wenye ulemavu kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa kutenga fedha za stahiki mbalimbali na vitendea kazi.
Aidha aliongeza kuwa vipaumbele vingine ni ujenzi wa shule mpya ya mchepeo maaluma wa kiingereza katika kata ya Nduli, kuboresha shughuli za utalii katika eneo la Kihesa Kilolo na Tungamalenga na kuboresha masuala mtambuka kama lishe na Ukimwi.
Aidha vipaumbele vingine vya halmashauri ni kuendeleza miradi mikakati kwa ajili ya kuongeza mapato ikiwemo mradi wa ujenzi wa maduka katika eneo la stendi ya zamani, kuboresha masoko ya Mwangata, Ipogolo, Njiapanda ya Mlowo na mradi wa samaki katika bwawa la Kihesa Kilolo.
Aidha manispaa imeweka kipaumbele katika kukamilisha shule mpya za sekondari za Igumbilo, Isakalilo na shule ya msingi Kipululu, ujenzi wa madarasa katika shule za msingi na sekondari na kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga wodi ya wagonjwa katika hospitali za Frelimo,Ipogolo, Itamba na kukamilisha kituo cha afya cha Mkimbizi na Mgongo.:
0 comments:
Post a Comment