Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiwahutubia wananchi, kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Wiki ya Asasi
Zisizo za Kiserikali 2019, yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri,
jijini Dodoma, Novemba 4.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
…………………………
*Ataka fedha wanazopata zitumike kujenga miradi mikubwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Asasi za Kiraia ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
“Nitoe rai kwenu wana AZAKI,
muendelee kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo
ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ili Serikali iweze kujenga miradi
mikubwa ya kijamii,” amesema.
Ametoa wito huo leo jioni
(Jumatatu, Novemba 4, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na
washiriki wa Maonesho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini
yaliyoanza leo kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Maonesho hayo
yatafikia kilele chake Ijumaa, Novemba 8, mwaka huu.
Amesema Serikali inatambua na
kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya Kiserikali katika kusukuma
gurudumu la maendeleo nchini kama vile kuwajengea uwezo viongozi wa
Serikali za Mitaa wakiwemo Madiwani, viongozi wa vijiji na mitaa ili
watambue majukumu yao.
“Niwatoe hofu tu kwamba
Serikali inatambua mchango wenu wa kuhamasisha wananchi kushiriki
shughuli mbalimbali za maendeleo; kujiongezea kipato na kupata ujuzi;
utoaji wa huduma za kijamii hususan elimu, afya, upatikanaji wa maji,
huduma za kisheria na huduma za mikopo midogo.
“Pia tunatambua mchango wa
AZAKI wa kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa wananchi pale mnapoona
kuna uhitaji. Pia mnaisaidia Serikali kupinga mila potofu na kandamizi
hasa kwa makundi yenye mahitaji maalum,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kuzitaka AZAKI nchini zizingatie sheria iliyofanyiwa
marekebisho ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24/2002 na kanuni
zake, ambayo ilipitishwa na Bunge kupitia Sheria Na. 3/2019 na
kusisitiza kwamba marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta hiyo.
“Nipende kuwahakikishia
wana-AZAKI kuwa marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta ya NGOs na
siyo kuyabana mashirika yasiyo ya Kiserikali kama ambavyo imekuwa
ikipotoshwa na baadhi ya watu. Marekebisho hayo yalizingatia misingi ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” amesema.
Kuhusu mapato ya AZAKI, Waziri
Mkuu amesema fedha wanazopata zinaweza kufanya miradi mikubwa ambayo
itawanufaisha wananchi na akawasihi wazitumie kwenye ujenzi wa miradi
mikubwa inayoonekana badala ya kuendesha semina na warsha.
“Tunajua fedha mnazopata
zinaweza kusaidia kwenye miradi hii. Kwa mfano, kuanzia Januari hadi
Septemba, mwaka huu, tulifanya mapitio ya ufadhili wa fedha mnazopata.
Na katika upekuzi uliofanyika kwenye taasisi 92, ilibainika kwamba
zilipokea jumla ya sh. bilioni 261.059 ambazo zimeingia kwenye AZAKI
hizi.”
“Vilevile, mwaka 2016 hadi
2017, tuliangalia mapato ya NGOs 51, tukagundua kuwa katika kipindi cha
miaka miwili, zimepokea jumla ya shilingi trilioni 2.5. Kama fedha hizi
zote zingeratibiwa vizuri kwa kupunguza matumizi yasiyo na umuhimu ni
lazima tungefika mbali. Tutumie vizuri fedha hizi za ufadhili kwa miradi
inayoonekana,” amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu ajira kwa
vijana, Waziri Mkuu amesema vijana ni kundi lenye umuhimu mkubwa katika
kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo licha ya kuwa wanakabiliwa
na uhaba wa ajira.
Amesema Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012, inaonesha asilimia 35 ya Watanzania wote ni vijana
wenye umri wa miaka 15 hadi 35. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa
nguvukazi ya Taifa wa mwaka 2014, vijana wamebainika kuwa ndio kundi
kubwa la nguvukazi ya Taifa ambao ni asilimia 56 ya nguvukazi yote
nchini.
“Kila mwaka, kumekuwa na
ongezeko la vijana wanaoingia kwenye soko la ajira. Kwa mfano, taarifa
ya hali ya ajira ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa mwaka 2019
inaonesha kuwa asilimia 11.8 ya nguvukazi ya vijana duniani ambao ni
takriban vijana million 59.1 hawana kazi,” amesema.
Mapema, Waziri wa Nchi
(OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alizishukuru asasi zote za kiraia
ambazo zinafanya kazi Tanzania kwa sababu zinawahudumia wananchi kwa
karibu zaidi. “Ninazishukuru NGOs zote kwa kusaidia kutoa elimu kwa
wananchi.
Tunazishukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya Tanzania nzima kwa
kushirikiana na Ofsi ya Rais TAMISEMI,”
Akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema mwaka huu,
wizara yake imesajili mashirika yasiyo ya Kiserikali 617 ikilinganishwa
na mashirika 385 yaliyosajiliwa mwaka 2017.
“Kati ya hayo mashirika 617,
mashirika 44 ni ya ngazi ya kimataifa; 551 ni ngazi ya kitaifa, saba ni
katika ngazi ya mikoa na mashirika 15 ni katika ngazi ya wilaya. Hadi
kufikia Oktoba, 30, 2019, tumeshasajili mashirika 19,318” alisema.
0 comments:
Post a Comment