METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 6, 2019

WAZIRI HASUNGA AVITAKA VYAMA VYA USHIRIKA KUAGIZA MBOLEA KWA PAMOJA

Waziri wa Kilimo Mhe Japht Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kwa wenyeviti na mameneja wa vyama vikuu vya ushirika wa kahawa, tumbaku, chai, miwa na mazao mchangayiko yaliyofanyika Jijini dodoma novemba 05, 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japht Hasunga (Mb) akiongoza kikao kazi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kwa wenyeviti na mameneja wa vyama vikuu vya ushirika wa kahawa, tumbaku, chai, miwa na mazao mchangayiko yaliyofanyika Jijini dodoma novemba 05, 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japht Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kwa wenyeviti na mameneja wa vyama vikuu vya ushirika wa kahawa, tumbaku, chai, miwa na mazao mchangayiko yaliyofanyika Jijini dodoma novemba 05, 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japht Hasunga (Mb)  akiwa katika picha ya pamoja na wenyeviti na mameneja wa vyama vikuu vya ushirika wa kahawa, tumbaku, chai, miwa na mazao mchangayiko wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kwa yaliyofanyika Jijini dodoma novemba 05, 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Pamoja na Serikali kusisitiza wakulima kuvitumia Vyama vya Ushirika katika utatuzi wa changamoto za kiuchumi na Kijamii, bado wanaushirika wameshindwa kubuni mfumo madhubuti wa kuwaunganisha katika ununuzi wa Pembejeo ambazo zingewapa unafuu wa gharama za uzalishaji pamoja na kwamba Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, kusisitiza kwamba Ushirika ni chombo pekee cha kumletea mwananchi mnyonge maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Kilimo Mhe Japht Hasunga (Mb) ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kwa wenyeviti na mameneja wa vyama vikuu vya ushirika wa kahawa, tumbaku, chai, miwa na mazao mchangayiko iliyofanyika Jijini dodoma novemba 05, 2019

Alisema kuwa pamoja na mafanikio ya Ushirika katika kutatua changamoto za kiuchumi za wanachama wake na wakulima, bado kumekuwa na changamoto za kuwepo kwa gharama kubwa za upatikanaji wa Pembejeo kutokana na Vyama vya Ushirika wa aina moja kuwa na njia zake za kupata Pembejeo.

Hivyo, ili kuondokana na gharama kubwa za upatikanaji wa mbolea na kuleta tija katika uzalishaji, Serikali imeanzisha mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS – Bulk Procurement System)kupitia Kanuni za Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer (Bulk Procurement) Regulations, 2017).

Lengo la mfumo huo ni ili wakulima wawezekunufaika na punguzo la bei litokanalo na ununuzi na usafirishaji wa mbolea nyingi kwa wakati mmoja (Economies of Scale).

Katika Mafunzo hayo Mhe Hasunga amewataka washiriki hao kuagiza mbolea kupitia BPS, ambapo watatakiwa kupata mahitaji ya jumla ikiwa ni pamoja na dhamana za Benki (Bank Guarantees) zinazowezesha kupata mbolea na kulipia ndani ya siku 180 kwa tozo ndogo tu za benki za asilimia 1 hadi 2 baada ya kufungua muamana (LC – Letter of Credit).
Pamoja na kwamba BPS inawalenga zaidi wakulima, bado kuna changamoto ya wakulima wadogo kupitia Vyama vyao vya Ushirika kutoshiriki katika BPS kwani tangu kuanza kwa BPS mwaka 2017, uagizaji wa mbolea kupitia BPS umekuwa ukitumiwa na wafanyabiashara wakubwa peke yake na, wanapoifikisha mbolea kwa wakulima na kuwakuta hawana fedha za kununua mbolea, wakulima hao hulazimika kuwekewa dhamana za mikopo (Credit Guarantees) na wanunuzi wa mazao na/au wenye viwanda vya mazao ya kilimoili wapate mikopo ya Benki yenye riba kubwa (asilimia 15 – 20 ya fedha iliyokopwa).

“Gharama za usambazaji nchini ni kubwa sana ikilinganishwa na gharama za kuingiza mbolea nchini. Jambo hili limekuwa likiwafanya wakulima wadogo wapate mbolea kwa bei kubwa sana kutokana na faida kubwa za wafanyabiashara, riba za mabenki na mifumo ya uingizaji wa mbolea nje ya BPS isiyo na uwazi na hivyo kufanya hata bei ya mbolea kwa wakulima kuwa kubwa kuliko uhalisia wa gharama ” Alisisitiza Mhe Hasunga


MBOLEA YA UREA

Katika zabuni ya uingizaji wa mbolea aina ya Urea kupitia BPS iliyofanyika Julai 04, 2019;bei ya mbolea katika chanzo ilikuwa US$ 275 na bei ya kusafirisha baharini  na bima ilikuwa US$ 29 kwa tani 1. Hii ilifanya gharama ya kufikisha mfuko mmoja wa mbolea bandari ya DSM iwe Tshs 34,500/=. Kama nilivyozungumza siku ya kutangaza bei elekezi kwa mbolea ya Urea, gharama ya kutoa mfuko mmoja bandarini, kuufungasha, kuusafirisha hadi kwa mkulima na faida za wafanyabiashara hadi Sumbawanga ni Tshs 22,500/=. Hii inafanya bei ya mkulima wa Sumbawanga iwe Tshs 57,000/=.

Kwa lugha nyingine, gharama ya kufikisha mbolea kwa mkulima ni asilimia 60 ya gharama za kuufikisha mzigo bandari ya Dar es salaam (CIF). Ukubwa wa gharama hizi umechangiwa sana na faida za wafanyabiashara (Tshs 6,700/= ambayo ni zaidi ya mara mbili ya gharama za kusafirisha mzigo hadi bandari ya DSM). Gharama hii ingeweza kuepukika kama vyama vya ushirika vingeagiza mbolea moja kwa moja kwa kutumia dhamana za benki.

Gharama zingine zinazochangia kwenye kuongezeka kwa bei ya mkulima ni kukosekana kwa mfumo wa uratibu wa usaifirishaji wa mbolea kutoka DSM hadi kwa mkulima. Kwa sasa mbolea husafirishwakwa kutumia mikangafu/malori yanayobeba mzigo mdogo wa tani 30 kwa Tshs 5,500/= kwa km 1,000.Hii ni karibu mara mbili ya gharama za kuusafirisha mfuko huo kutoka kwenye chanzo (Tshs 3,336/= kutoka Qatar ambayo iko zaidi ya km 5,000 kutoka bandari ya DSM). Gharama hizi zingepungua endapo usafiri wa Reli ungetumika.

Aidha, kutokana na riba za Benki (asilimia 20 au Tshs 11,400/=), mkulima hulazimika kulipa Tshs 68,400/=. Endapo vyama vya ushirika vitaingia katika BPS, gharama hii itaepukika.

Pamoja na kuepuka gharama za usafirishaji kwa kutumia mikangafu badala ya reli, faida kubwa za wafanyabiashara na riba za mabenki, bei ya mbolea aina ya urea kwa wakulima itashuka kwa takriban Tshs 8,000/= ikilinganishwa na bei elekezi zilizopo.
MBOLEA YA DAP
Waziri Hasunga alisema kuwa Pamoja na kwamba, wakati wa ufunguaji wa zabuni kupitia BPS uliofanyika Juni 21, 2019, bei ya mbolea ya kupandia (DAP) iilkuwa kubwa sana katika soko la Dunia (US$ 350 - 380) na bei za mbolea aina za NPK ilikuwa ndogo sana (US$ 265 – 300), bado mbolea za NPK hapa nchini zimekuwa na bei kubwa sana ikilinganishwa na bei za mbolea aina DAP ambayo ni Tshs 58,000 hadi 60,000/= katika mikoa ambako tumbaku huzalishwa (Tabora, Katavi, Ruvuma na Mbeya). Bei ya NPK ya tumbaku katika mikoa hiyo hiyo ni US$ 34.5 (Sawa na Tshs 79,400). Kwa vile wakulima hupewa kwa mikopo ya mabenki, hulipa fedha hizo pamoja na riba (asilimia 7 – 10) na hivyo kufanya mkulima ainunue mbolea hiyo kwa Tshs 85,700/=.
Ili mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja uweze kunufaisha wakulima wadogo kwa kupunguza bei za mbolea kwa kadri inavyowezekana Waziri Hasunga ameagiza Vyama vikuu vya ushirika kuratibu ukusanyaji wa mahitaji ya mbolea kutoka kwenye vyama vya msingi (AMCOS) kwa wakati na kutathmini gharama zitakazohitajika, Vyama vikuu vya ushirika vihakikishe kwamba vinatunza kumbukumbu sahahi za mahesabu ili hati za ukomo zitolewe kwa wakati ili kurahisisha upatikanaji wa dhamana za Benki.
Maagizo mengine ni pamoja na Mrajis wa ushirika kusimamia mchakato mzima wa upatikanaji wa ukomo wa madeni ili kurahisisha upatikanaji wa dhamana za Benki kwa wakati, wauzaji wa mbolea kuwa mawakala wa vyama vya ushirika na/au viwanda (mahali inapohitajika) ili kurahisha zoezi la utoaji wa mbolea bandarini na kuisambaza kwa wakulima, na Mbolea zote zitasafirishwa nchini kwa pamoja (Bulk Domestic Distribution)

Kadhalika Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameagiza Usafiri wa Reli utatumika badala ya barabara. Kikotoo cha bei elekezi kimechukulia usafiri wa mikangafu (Trucks) kwa Tshs 5,500 kwa km 1,000. Gharama hii inaweza kupungua endapo mbolea itasafirishwa kwa reli kwa Tshs 4,160 (TRC) au Tshs 4,600 (TAZARA). Gharama hii inaweza kupungua zaidi kama mbolea nyingi itasafirishwa kwa wakati mmoja.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com