WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020/2021 umelenga kutekeleza
maeneo ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na kufungamanisha ukuaji wa uchumi
na maendeleo ya watu kwa kuweka mkazo katika upatikanaji wa huduma bora
za jamii ikiwemo elimu, maji, afya, umeme na barabara.
Ametaja maeneo mengine
ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda kwa kuimarisha sekta ya kilimo
kwa kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi inayopatikana nchini,
kuimarisha mashirika ya viwanda na kuanzisha na kuendeleza maeneo ya
viwanda.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Ijumaa, Novemba 15, 2019) wakati akiahirisha mkutano wa 17 wa Bunge la
11 jijini Dodoma. Amewasisitiza wananchi kutekeleza majukumu yao kwa
weledi, uadilifu na uzalendo ili kuiwezesha nchi kufikia malengo ya
kujenga uchumi imara, unaojitegemea na wenye kuweza kuhimili ushindani.
“Ujenzi wa mazingira wezeshi
katika kuendeleza miundombinu itakayosaidia maendeleo ya biashara na
uwekezaji nchini; kuhakikisha Watanzania wenye sifa stahiki wanapewa
kipaumbele katika kandarasi au ajira zinazotokana na utekelezaji wa
miradi ya kimkakati.”
Amesema eneo lingine ni
kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Mpango. Baada ya tathmini ya
utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2016/2017–2020/2021 kwa lengo la kuimarisha usimamizi na kuanza
maandalizi ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
(2021/2022–2025/2026).
Kadhalika, Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kusisitiza Maafisa Masuuli wazingatie maeneo ya
kipaumbele yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na
wahakikishe kamati za mipango na bajeti katika mafungu yao zinatekeleza
majukumu yake ipasavyo.
“Serikali kwa upande wake itaandaa mipango ya
kisekta, kitaasisi na kimaeneo ambayo utekelezaji wake utachochea ujenzi
wa uchumi wa viwanda, mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.”
“Katika udhibiti wa matumizi,
naendelea kuwasisitiza Maafisa Masuuli wahakikishe wanatumia mfumo wa
kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (Tanzania National Electronic
Procurement System – TANePS). Hivyo, kila taasisi ya nunuzi ihakikishe
inatumia mfumo huo kabla ya tarehe 31 Desemba 2019.
Waziri Mkuu amesema Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa
upande wake itaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta zinazogusa
wananchi moja kwa moja na kuhakikisha kuwa matunda ya kukua kwa uchumi
yanawafikia wananchi.
“Watanzania wanatakiwa
kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli,
katika kipindi hiki ambacho amekuwa akichukua hatua za makusudi
kuhakikisha anajenga uchumi imara, kuboresha kipato na hali ya maisha ya
wananchi.”
Amesema matunda ya maboresho
hayo yanayoendelea yanaonekana katika maeneo mengi. “Ndani ya miaka 26
kuanzia 1991/1992 hadi 2017/2018 kiwango cha umaskini wa mahitaji ya
msingi kimeweza kupungua kwa asilimia 13. Kadhalika, umaskini wa chakula
nao umepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka
2017/18.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amesema katika kuelekea msimu wa kilimo wa 2019/2020 hali ya upatikanaji
wa chakula nchini imeendelea kuimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa
mazao ya chakula kwa msimu 2018/2019, ambao ulifikia tani milioni 16.41
ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.84 na kuiwezesha nchi
kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula kwa asilimia 119.
Amesema pamoja na uzalishaji
huo mzuri, kumekuwepo na mahitaji makubwa ya nafaka katika baadhi ya
maeneo kutokana na hali ya mvua kutokuwa nzuri na kuwepo kwa dalili za
kupanda bei za nafaka, Serikali imetoa maelekezo kwa Wakala wa Hifadhi
ya Chakula ya Taifa kuhakikisha inasambaza nafaka kwenye maeneo yenye
upungufu ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei.
“Nitumie fursa hii kuwahimiza
wakulima kutumia vizuri mvua za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mengi
ya nchi yetu kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na ekolojia ya
maeneo husika. Aidha, tukumbuke pia kujiwekea akiba ya kutosha ya
chakula kwa ajili ya matumizi ya kaya baada ya mavuno badala ya kuuza
chakula chote.”
Kuhusu upatikanaji wa
pembejeo, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha wakulima wanapata
mbolea kwa wakati na bei nafuu, Serikali imetoa bei elekezi kwa mbolea
aina ya DAP na UREA ambazo zipo katika Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa
Pamoja. “Hivyo, nitumie fursa hii kuzikumbusha mamlaka husika
kuhakikisha kwamba bei elekezi zinafahamika kwa wakulima katika maeneo
yote na wauzaji wanauza kwa kuzingatia bei hizo.”
Pia, Waziri Mkuu amezungumzia
kuhusu masoko ya mazao ya kilimo ambapo amesema licha ya kuongezeka kwa
uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini, kumekuwepo na changamoto kadhaa
za upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa baadhi ya mazao ikiwemo la
pamba, korosho na tumbaku.
Amesema changamoto hizo
zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko na mwenendo wa bei katika
soko la dunia pamoja na uwezo mdogo wa kuchakata mazao hayo nchini,
hivyo Serikali inaimarisha mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo, mifugo
na uvuvi, kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa
kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Hatua hizi zitasaidia
kuongeza thamani ya mazao na hivyo, kuimarisha bei. Kwa sasa tunaendelea
na msimu wa mauzo wa zao la korosho baada ya mazao ya pamba na kahawa
kumaliza. Minada ya korosho inaendelea vizuri. Viongozi wa Mikoa na
Wilaya wasimamie malipo kwa wakulima na kuhakikisha wanalipwa kwa
wakati.”
0 comments:
Post a Comment