Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza mkakati wa serikali katika kukabiliana na Sumukuvu nchini wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumkuvu (Alfasafe) kwenye vyakula uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha tarehe 4 Novemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumukuvu (Alfasafe) kwenye vyakula wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akisisitiza mkakati wa serikali katika kukabiliana na Sumukuvu nchini, uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha tarehe 4 Novemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akifuatilia mawasilisho mbalimbali ya washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumukuvu (Alfasafe) kwenye vyakula uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha tarehe 4 Novemba 2019.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumukuvu (Alfasafe) kwenye vyakula wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akisisitiza mkakati wa serikali katika kukabiliana na Sumukuvu nchini, uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha tarehe 4 Novemba 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Hivi karibuni, Serikali ya Tanzania
ilipata fedha za kutekeleza mradi wa kuzuia kuenea kwa sumukuvu hapa nchini
(TANIPAC). Mradi huo unalenga kupunguza kutokea kwa madhara ya sumukuvu katika
mfumo wa chakula kupitia udhibiti husishi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao
ya mahindi na karanga, hivyo kuboresha uhakika na usalama wa chakula na hatimae
kuimarisha afya na lishe ya jamii yetu na kuimarisha biashara kati ya Tanzania
na nchi zinazotuzunguka.
Mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia
mkakati Madhubuti kwa kushughulikia masuala yote yanayohusu sumukuvu hapa
nchini. Mkakati huo unazingatia udhibiti wa sumukuvu katika hatua za
uzalishaji, uvunaji, udhibiti wa kibilojia, teknolojia baada ya kuvuna na njia
za ukaushaji, uhifadhi, kujenga uwezo wa kitaasisi, uratibu na kutoa elimu ya
kuhamasisha wadau muhimu. Ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika
uhaulishaji wa teknolojia pamoja na kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga
(Mb) ameyasema hayo leo tarehe 4 Novemba 2019 wakati akifungua Mkutano wa
kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumkuvu (Alfasafe) kwenye vyakula uliofanyika
katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha.
Mhe Hasunga amesema kuwa Ushirikiano
wa kiutafiti, kati ya sekta binafsi na watunga sera, ni muhimu katika kufanikisha
mageuzi ya kilimo.
Waziri Hasunga amesema kuwa Tangu
kuibuka kwa tatizo la sumukuvu mwaka 2016, Tanzania imechukua hatua mbalimbali
za kupunguza kusambaa kwa sumukuvu hapa nchini. Kwa kutambua changamoto za
kukabili sumukuvu, ambapo kunahitajika kutumia njia mbalimbali kuanzia kwenye
hatua za uzalishaji, uvunaji, uhifadhi, usindikaji na kuhusisha sekta za Umma
na Binafsi katika kupunguza upotevu wa chakula na kuongeza upatikanaji wa
chakula salama na lishe bora.
Amesema, Tanzania imeanzisha Kamati
Jumuishi ya Uendeshaji inayohusisha sekta na taaluma kutoka taasisi mbalimbali
chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Kilimo ambayo ina mamlaka ya kusimamia masuala
yote yanayohusu sumukuvu.
Kadhalika, amewahakikishia washiriki
hao kuwa kinga ya sumukuvu - Alfasafe TZ01; imeshasajiliwa kwa matumizi
hapa nchini Tanzania. "Aidha, nimefarijika kuwa kazi hii inafanywa
na Kampuni Binafsi ambayo imewekeza katika uzalishaji, na usambazaji wa bidhaa
hii ambayo itaokoa Maisha ya watu hapa nchini" Alisisitiza
"Napenda kuwahakikishia utayari
wa Wizara yangu katika kuyatumia maazimio mtakayokubaliana katika mkutano huu.
Aidha, Serikali ya Tanzania, inatilia maanani na inaunga mkono hatua
zinazochukuliwa katika kuhimiza biashara ya chakula salama, usalama wa chakula na
lishe" Alisema Mhe Hasunga
Tanzania kwa sasa inatekeleza Awamu
ya Pili Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo (ASDP II) yenye lengo la
kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo kuwa na kilimo chenye tija na kibiashara,
pamoja na kukuza uchumi wa wakulima wadogo na kuboresha maisha, uhakika wa
chakula na lishe bora.
Uhakika wa chakula na lishe ni
muhimili ambao ni muhimu wa ASDP II Katika kufikia malengo hayo, uwekezaji
katika utafiti wa kilimo ni muhimu katika kuleta matokeo kwa wakulima na wadua
wengine katika mnyororo wa thamani.
Waziri Hasunga amesema kuwa kutokana
na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) za mwaka
2017, Tanzania inaongoza katika uzalishaji wa mahindi na karanga katika ukanda
wa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuzalisha tani milioni 6 na tani milioni moja
mtawalia.
Amesema, Pamoja na mafanikio hayo,
Serikali inatambua kuwa, ingawa mazao hayo ni muhimu kwa chakula cha kila siku,
lakini yanakabiliwa na ukubwa wa tatizo la sumukuvu ambalo linahatarisha
usalama wa chakula na kuwa kikwazo cha biashara ya mazao hayo kwa nchi jirani
na Tanzania.
Mkutano huu ambao umewaweka pamoja
watafiti, wafanyabiashara, watunga sera na wadau wa maendeleo, ambao unalenga
kupanga mikakati ya kuongeza kasi ya matumizi ya kinga ya sumukuvu (Alfasafe),
na kukabili sumukuvu barani Afrika, unadhihirisha mabadiliko chanya ya
kimtazamo tunayoyahitaji.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment