METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 19, 2019

MIRADI 6 YAZINDULIWA NA MWENGE WA UHURU WILAYANI BAHI


Na.Alex Mathias,Bahi
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 Mzee Mkongea Ally amezindua na kuweka mawe ya msingi miradi 6 yenye thamani ya sh bil 8.7 katika halmashauri ya Bahi huku akiwataka viongozi na wananchi kuilinda miradi hiyo ili idumu.
Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa maboma manne katika shule ya sekondari ya Mundemu uliowekwa jiwe la msingi,mradi wa usambazaji maji kijiji cha Mkakatika na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya km 2.3 katika mji wa Bahi ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyowahi kuitoa Rais dkt John Magufuli wakati wa kampeni 2015.
Akizungumza  baada ya kukagua miradi hiyo Mkongea amesema Rais Dkt John Magufuli anatumia fedha nyingi kupeleka kwenye miradi ili iwasaidie wananchi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuilinda.
“Katika mradi huu wa maji wa Mkakatika tumetumia muda mrefu kujiridhisha ili tuone thamani ya fedha, na baada ya ukaguzi huo tumeridhishwa na natamka kwamba Mwenge wa Uhuru 2019 umeridhia kuweka jiwe la msingi mradi huu,”amesema Mkongea.
Pamoja na kuridhia kuweka jiwe la msingi ametoa maelekezo ikiwemo kuhakikisha mkandarasi wa ujenzi anapeleka vipimo katika maabara ya serikali.
“Mradi huu nimeambiwa bado haujakamilika, hivyo nisisitize mambo mawili, moja kuhakikisha fedha zilizobaki zinatumika kukamilisha mradi huu, pili mkandarasi ahakikishe anapitisha vipimo vyote katika maabara ya serikali,”ameongezea Mkongea.
Akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya Mkongea amewapongeza na kusema ujenzi huo umetekelezwa vizuri na thamani ya fedha imeonekana.
Amesema ametembelea ujenzi wa hospitali nyingi zilizopewa sh bil 1.5 lakini nyingine bado ndio wanapaua na kusema kuwa Bahi ni hospitali ya kwanza kati ya zote alizotembelea.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amewashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
“Mafanikio tunayoyapata yanatokana na ushirikiano wa wananchi na ushirikiano uliopo baina yetu sisi watumishi, tukuahidi kufanyia kazi maelekezo yote,”alisema Mkuu wa wilaya huyo
Mwenge wa Uhuru pia ulitembelea mradi wa utunzaji wa chanzo cha maji na uhifadhi wa msitu wa Chenene uliopo kijiji cha Mayamaya, uliweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha kokoto katika kiwanda cha kokoto cha kampuni ya KASCCO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com