METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 18, 2019

TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA KUSAJILI MAAFISA USHIRIKA


Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Jijini Dodoma, hivi karibuni

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani amesema Tume inaazimia kusajili Maafisa Ushirika nchini kote kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na kuimarisha utendaji wa Sekta ya Ushirika ili Wanaushirika pamoja na Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika na Ushirika.

Akizungumza wakati wa Kikao cha Watumishi kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma Dkt. Kamani amesema Tume ina dhamana ya Kusimamia Sekta ya Ushirika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013. Hivyo, ni wajibu wa Tume kuhakikisha kuwa ina rejesta ya usajili wa Maafisa Ushirika katika ngazi za Wilaya, Majiji na Manispaa ili kuongeza ufanisi na tija katika ufuatiliaji wa utendaji kazi wao.

“Tunakwenda kusajili Maafisa Ushirika wa ngazi zote na hili litafanyika ili pale ambapo Tume inapotoa maagizo na maelekezo ya utekelezaji iwe rahisi kufuatilia na kumuwajibisha kila muhusika kwa kadri ya nafasai na jukumu lake. 

Hii itaturahisishia hata pale panapojitokeza ubadhilifu na ukiukaji wa taratibu za kiushirika Watendaji kuanzia Maafisa Ushirika wa ngazi husika palipotokea ukiukaji huo kuwajibika kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu husika na hatua ziweze kuchukuliwa,” alisema Dkt. Kamani

Aidha, Mwenyekiti ametaja Sekta ya Ushirika kuwa ni moja ya maeneo muhimu ambayo yana fursa kubwa katika kushiriki na kuendeleza Uchumi wa Tanzania kupitia maendeleo ya Viwanda ili kuifikisha nchi katika Uchumi wa kati ifikapo 2025 na kuongeza kuwa Ushirika ina rasilimali nyingi zinazoweza kuwa ni nyenzo muhimu katika uanzishaji wa Viwanda kupitia malighafi zinazotokana na mazao ya Kilimo, uvuvi, madini na ufugaji. 

Kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo katika Sekta hii inayogusa maslahi ya wananchi ni Dhahiri kwamba Tume lazima iweke udhibiti na usimamizi makini wa ufuatiliaji wa kazi zinazofanywa na watendaji wa Sekta ya Ushirika katika ngazi zote kuanzia Maafisa Ushirika waliopo maeneo mbalimbali nchini.

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti aliwataka watumishi kuwa wabunifu katika kusaidia kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na wanaushirika ili kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuendeleza uchumi wa viwanda. 

Akiongeza kuwa Ushirika ni fursa kwa Viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali ya Kilimo, uvuvi, madini na mengine. Akiongeza kuwa viwanda hivyo vianzishwe kwa malengo ya kutoa suluhu ya changamoto katika Sekta ya Ushirika akitolea mfano eneo la vifungashio vya mazao eneo ambalo bado lina uhitaji mkubwa nchini.

“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuchangia mawazo na utekelezaji wa maeneo ya kuendeleza, kuanzisha au kuboresha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. Hivyo kuongeza mnyororo wa thamani,” alisema Dkt. Kamani

Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea katika kikao hicho alisema baada ya Vyama 4,413 kukaguliwa na Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika hivi karibuni Tume ichukue fursa hiyo kuendelea kuboresha taswira ya Sekta ya Ushirika kwa kutumia matokeo ya kaguzi zilizofanyika kwakuwa kaguzi hutoa picha na muelekeo wa utendaji.

“Tuongeze hamasa na elimu ya Ushirika kwa wale ambao bado hawajajiunga na Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na Ushirika ili kupitia Ushirika ili wananchi waweze kupata maendeleo kwa urahisi pamoja na kunufaika na viwanda kupitia Sekta ya  Ushirika. Watumishi niwaombe muendelee kuandika mapendekezo mbalimbali yenye lengo la kutafuta ushirikiano na wadau wa maendeleo ili tukuze na kuendeleza viwanda vya Ushirika,” alisema Dkt. Ndiege   

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu Bw. Athanas Mutwe akiongelea masuala ya kiutumishi katika kikao hicho alisema Watumishi ni kiungo muhimu sana chenye mchango mkubwa katika kuendeleza Sekta ya Ushirika na hatimaye kufikia Tanzania ya Viwanda.  Bw. Mutwe aliwataka watumishi hao kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma kwa manufaa yao binafsi na Taifa lote.

“Niwaombe watumishi wote kila mmoja wetu kuzingatie maadili ya utumishi wa Umma, tufanye kazi tukijua tumepewa dhamana ya kusimamia rasilimali na sekta muhimu ya Ushirika,” alisema Mutwe 

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilitoa fursa kwa watumishi wa Tume kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko ya Kisheria yatakayounda Sheria ya Ushirika   inayotarajiwa kujadiliwa Bungeni mapema mwakani 2020.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com