METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 16, 2016

WAZIRI UMMY MWALIMU ATOA TAMKO KUHUSU HUDUMA ZA MATIBABU KWA WATU WENYE ULEMAVU WASIO NA UWEZO

ummy-mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu anapenda   kutoa ufafanuzi kuhusu Tamko la Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) kuhusu makundi ya wananchi wanaostahili kupata msamaha wa matibabu. Aidha, baadhi ya Vyombo vya habari vimenukuu maelezo  ambayo yametolewa na mwenyekiti wa SHIVYAWATA kuhusu  Makundi yanayostahili kupata msamaha wa Matibabu nchini.

Kutokana na Maelezo hayo, napenda kutoa ufafanuzi ufuatao;  Sera ya Afya ya Mwaka (2007) inatambua kuwa wapo wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuzifikia huduma za Afya  wakiwemo  watu Wenye Ulemavu. Aidha, Kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu  Na.9/2010 ambayo, pamoja na mambo mengine, Sheria inabainisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wana haki ya kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za Afya.

Kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Afya (2007) na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu(2010) Wizara yangu inatambua na  itaendelea kuhakikisha kwamba Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kugharamia  huduma za Matibabu wanapatiwa Msamaha wa Matibabu katika Ngazi zote kuanzia Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Mikoa na Hosptali za Rufaa. Pia kwa kutambua umuhimu wa huduma ya Afya kwa Wananchi wote, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika mchakato wa kutungwa kwa sheria itakayowezesha wananchi wote wakiwemo Watu Wenye Ulemavu kupata Kitambulisho cha Bima ya Afya. Hatua hii itawaondolea vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu Wenye Ulemavu katika kuzifikia huduma za Afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.

Naomba kuchukua fursa hii kuwahakikishia ndugu zangu Wenye Ulemavu kuwa wanayo haki ya kupata huduma za matibabu katika ngazi zote. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha  makundi maalum  wakiwemo watu Wenye Ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma za Matibabu wanapata msamaha wa matibabu katika  vituo  vyote vya kutolea huduma za afya.

Natoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za  Mitaa kuwatambua Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kuchangia huduma za matibabu na kuimarisha Kitengo cha Huduma za Ustawi wa Jamii katika  vituo vya kutolea huduma za Afya ili viweze kuwatambua  na kutoa msamaha kwa watu wenye ulemavu wasio na uwezo ili  waweze kupatiwa matibabu bila ya vikwazo vya ukosefu wa fedha.

Aidha,  ni marufuku kwa Mtumishi yeyote wa Sekta ya Afya kuonesha vitendo vyovyote vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa Watu Wenye Ulemavu wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za  afya. Mtumishi atayethibitika kuonesha kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za Afya kwa kufanya vitendo vya vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi maaalum ikiwemo  watu wenye ulemavu  atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
 
Wizara yangu inafanya jitihada kuhakikisha kuwa inaondoa vikwazo vyote vinavyowanyima watu wenye ulemavu kupata huduma za afya wanazohitaji ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowawezesha kufika hospitali kwa kuweka miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Vile vile, ninawataka watoa huduma wote kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu wanapofika  hospitali. Wapatiwe huduma haraka ili kuwapunguzia usumbufu kutokana na mahitaji yao ya kimwili. Kama ambavyo tumefanya kwa Wazee niwaagiza kila kiongozi ahakikishe anaweka utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya kwanza watu wenye ulemavu tukijifunza kwa jinsi tulivyofanya na kufanikiwa katika eneo la kuhudumia wazee.

Watu wenye ulemavu ni wenzetu, watoto wetu, ndugu na jamaa zetu. Tuwahudumie kwa upendo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na wengine

Imetolewa na
MHE. UMMY A. MWALIMU (Mb.)
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto
15/10/2016 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com