Afisa wa TRA akimuelimisha mfanyabiashara huhu (kulia) katika
stendi ya mabasi Ikwiriri, Wilayani Rufiji Mkoani Pwani leo Novemba 13, 2019
kuhusu elimu ya kodi katika maduka yao mtindo unaotumiwa na TRA kutoa elimu ya
kodi unajulikana kama "Duka kwa Duka"
Na Mwandishi wetu, Rufiji
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani Juma Njwayo amepongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za kutoa elimu ya Kodi kwa kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao "duka kwa duka".
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa aina hii ya utoaji elimu ya kodi kwa kuwafuata wafanyabiashara utaongeza ari ya ulipaji kodi miongoni mwa wafanyabiasha na walipakodi wengine siyo tu katika Wilaya ya Rufiji bali hata kwa watanzania wote.
"Niwapongeze sana TRA kwa kuamua kufanya wiki ya elimu na huduma kwa walipakodi katika Wilaya yetu, naamini wana Rufiji tutafaidika na elimu hii na mapato yataongezeka", amesema DC Njwayo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka wafanyabiasha na wananchi wa Wilaya ya Rufiji kutumia fursa hii kufahamu mambo yanayohusu ulipaji kodi ili walipe kodi kwa hiari na kwa wakati na kuiwezesha serikali kutekeleza miradi mikubwa yenye tija kwa Taifa.
"Sote tunashuhudia jinsi Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli anavyotekeleza miradi mikubwa kama huu wa kufua umeme wa Nyerere Hydro power tena upo wilayani kwetu, kwa hiyo tutumie fursa ya elimu ya kodi na kila mmoja aone ana wajibu wa kulipa Kodi kwa hiari ili tupate maendeleo zaidi", amesisitiza Mkuu wa Wilaya Njwayo.
DC Njwayo ameongeza kuwa Kodi zinazokusanywa na TRA ndizo zinazoleta maendeleo ukiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kitaifa kwa kutumia Kodi mradi wa umeme ambao utainua wilaya kiuchumi na kijamii pamoja na kuinua hali za wananchi.
Ameongeza kuwa ni vyema wananchi kushirikiana na TRA katika kuhakikisha kuwa elimu watakayoipata wanaifanyia kazi na kuchangia maendeleo ya taifa letu.
Naye Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Honesta Ndunguru ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Rufiji kwa ushirikiano waliouonesha na kuwa TRA itahakikisha inafika katika sehemu zote muhimu zenye wafanyabiasha na kuwasajili kuwa walipakodi na kuwapatia cheti Cha utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
"Tutatoa TIN kwa kila anayestahili kupata kwa ajili kufanya biashara au kupata huduma zingine kama vile leseni ya udereva", amesema Ndunguru.
TRA inafanya wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi katika mikoa ya Morogoro na Pwani kuanzia tarehe 11 hadi 16 ili kuongeza uelewa wa masuala ya ulipaji kodi miongoni mwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani, Mhe. Juma Njwayo (mwenye fulana nyeupe) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliofika ofisini kwake kutoa taarifa ya wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi inayoendelea katika wilaya hiyo iliyopo Mkoa wa Pwani
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma Njwayo (kushoto) akiagana na Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania waliofika ofisini kwake kutoa taarifa ya wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi inayoendelea katika wilaya hiyo.
0 comments:
Post a Comment