********************************************
Ubalozi wa Nchi za Falme za
Kiarabu UAE umeendelea kuunga mkono kampeni ya Upasuaji wa Moyo kwa
Watoto kutoka familia duni Iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul
Makonda ambapo leo October 31 wamemkabidhi hundi ya Shilingi Milioni 27
kwaajili ya Bima za Afya kwa Watoto 500 wenye Tatizo la Moyo.
RC Makonda amesema kiasi hicho cha
fedha kitawezesha Watoto 500 wakiwemo yatima na Wanaotokea familia duni
Waliolazwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kupata Bima za Afya
zitakazowawezesha kupata Matibabu Bure kwa kipindi cha Mwaka Mzima.
Aidha RC Makonda amesema uamuzi wa
kuwatafutia Bima za Afya umekuja baada ya kubaini Watoto wengi
wanaofanyiwa upasuaji wanahitajika kwenda Clinic kwaajili ya kufuatilia
maendeleo ya Afya na Dawa lakini kutokana ugumu wa maisha wanashindwa
kumudu gharama jambo linalowafanya Wazazi au Walezi wao kuuza Mali
walizochuma kwa muda mrefu ili wapate fedha na mwisho wa siku familia
inazidi kuwa maskini.
Pamoja na hayo RC Makonda
amemshukuru Balozi kwa kuendelea kumuunga mkono katika mambo mbalimbali
ikiwemo kusomesha watoto 100 wa kike kidato cha tano na sita, Kumpatia
madaktari bingwa wa Moyo Waliofanya upasuaji kwa watoto 60, Kumsaidia
futari kwaajili ya Maimamu wa Misikiti 800 huku akitoa wito kwa Wananchi
kuwa na moyo wa upendo wa kusaidia wenye uhitaji.
Kwa upande wake Balozi wa Nchi za
Falme za Kiarabu Bw. Khalifa Abdulrahman Almarzooqi amesema kuwa Ubalozi
huo unafurahishwa na kazi nzuri ya RC Makonda katika kusaidia Wananchi
wenye uhitaji ndio maana wameamua kushirikiana nae kwa kila jambo
kwakuwa kila msaada anaoupokea unawafikia walengwa.
0 comments:
Post a Comment