METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 18, 2019

Mkoa wa Lindi Wajivunia Mafanikio Miaka 4 ya JPM

Na Mwandishi Wetu, Lindi

Mkoa wa Lindi umetumia zaidi ya bilioni 10.4 zilizotolewa na Serikali ya Awamu  ya Tano katika kipindi cha miaka minne kuboresha sekta ya afya.

Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amesema kuwa baadhi ya miradi iliyonufaika na fedha  hizo ni pamoja na ujenzi wa Hosptali za Wilaya, Vituo vya Afya, na Zahanati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za afya.


“Ujenzi wa miundombinu katika sekta hii umeenda sambamba na upatikanaji wa dawa ambao umefikia zaidi ya asilimia 95 katika maeneo yote ya kutolea huduma katika mkoa wetu,” alisisitiza Zambi.


Akifafanua,amesema kuwa kuimarishwa kwa huduma za afya katika mkoa huo kumesaidia kuwawezesha wananchi kushiriki katika kukuza uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula, hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.


Akizungumzia elimu bure Mhe. Zambi amesema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 4 zimetolewa kugharamia elimu bure katika mkoa huo hali iliyowezesha kuongeza maradufu kiwango cha wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na shule za msingi.


Kwa upande wa chuo cha ualimu Nachinge, Mhe. Zambi amesema kuwa zimetumika kukarabati chuo hicho  kwa kuboresha miundombinu yake ikiwemo mabweni, maktaba na madarasa.


Katika sekta ya maji, Mradi wa Ngapa umewezesha uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 7.5 ikilinganishwa na lita milioni 2 zilizokuwa zikizalishwa awali kabla ya kutekelezwa kwa mradi huo.


Mhe. Zambi amebainisha kuwa mkoa huo umepiga hatua katika sekta ya uwekezaji kutokana na kuwepo kwa nishati ya uhakika baada ya mkoa huo kuunganishwa na gridi ya Taifa hali inayowezesha wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, gesi na uchimbaji wa madini.


“Mkoa wa Lindi umepata wawekezaji katika sekta ya uchimbaji wa madini ya graphite na bado tunaendelea kuwakaribisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza katika mkoa wetu kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu na upatikanaji wa umeme wa uhakika,” alisisitiza Zambi.


Mkoa wa Lindi ni moja ya mikoa iliyofanikiwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuleta mageuzi na ustawi wa wananchi katika sekta za afya, elimu, maji, barabara na nyingine zinazolenga kukuza uchumi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com