METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 2, 2019

KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO MATHEW MTIGUMWE ATISHIA KUWAFUTA WAKANDARASI MIRADI YA UMWAGILIAJI MOROGORO






Na Innocent Natai, TPRI, Morogoro

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, amewataka wakandarasi wa miradi ya Maghala na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji mkoani Morogoro kuhakikisha wanaikamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kuwasaidia wakulima na kuondoa changamoto za umwagiliaji na uhifadhi wa zao la mpunga.

Mtigumwe ameyasema hayo wakati akikagua utekelezwaji wa miradi ya ujenzi wa Maghala na ukarabati wa miundombinu ya Umwagiliaji kijiji cha Mvumi wilayani Kilosa na Msolwa Ujamaa wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Mradi unaojulikana kama Expanding Rice Production Project (ERPP) unaosimamiwa na Wizara ya kilimo, wenye lengo la kusaidia kuongeza Uzalishaji kwa wakulima wadogo wadogo wa Mpunga.

Mhandisi Mtigumwe amewataka watendaji na wakandarasi kuhakikisha kuwa wanafanya haraka kukamilisha miradi hiyo kabla ya muda uliopangwa wa kuisha kwa miradi hiyo mwezi wa nne mwaka 2020 kwani wananchi na wakulima wa mpunga wanaisubiri miradi hiyo kwa hamu ili kuwaondolea changamoto ya umwagiliaji na uhifadhi.

‘’Kuna makontrakta ambao mpaka sasa wapo nyuma kidogo katika ujenzi hasa wa ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji lakini hawa wa maghala wapo vizuri wanaweza wakamaliza katika muda uliopangwa hivyo ni jukumu lenu viongozi kuhakikisha tunawafuatilia hawa wa umwagiliaji na mimi ntakuwa nakuja kila mwezi kuona wamefikia wapi na pia wapewe barua za onyo haiwezekani muda wa mradi umekaribia kwisha alafu mkandarasi bado anasuasua” Alisema Mhandisi Mtigumwe.

Alisema ni usaliti kwa Nchi kupewa fedha za uzalishaji na ujenzi za ufadhili kutoka nje alafu baadhi ya wakandarasi wazembe wanazitumia vibaya na kushindwa kuzipeleka katika matumizi husika na kwa wakati husika bila kuchelewesha.


‘’Kabla  miradi hii kufikia katika hali mbaya nitawachukulia hatua kali za kisheria wakandarasi wanaochelewesha miradi, siwezi kuvumilia kuona miradi mibovu na inayocheleweshwa’’Aliongeza Mhandisi Mtigumwe
  
Ameongeza kuwa  utunzaji wa nafaka katika  sekta ya Kilimo umekuwa ni changamoto kubwa hivyo miradi hiyo ya maghala na umwagiliaji ikikamilika itasaidia katika maeneo ya mradi, kuboresha mapato na nchi na kukuza uchumi kwa wakulima.


Katika usimamizi wa mradi huu wizara tano zinahusika kwa upande wa Tanzania bara ikiwemo wizara ya Kilimo ambayo ndio msimamizi mkuu, Viwanda na Biashara kwa ajili ya masoko, TAMISEMI kwa sababu ya maeneo ya miradi inapotekelezwa  yapo chini ya  Halmashauri na Wilaya ambazo zipo chini ya TAMISEMI, Wizara ya Maji kwa ajili ya kusimamia hati za matumizi ya maji na Ofisi ya Makamu wa Rais mazingira kwa sababu usimamizi wa mazingira ya ujenzi wa miundombinu ya miradi

Mradi huu ulianza mwaka 2015 na kwa ujenzi wa maghala ulianza mwaka huu mwezi Aprili katika maeneo mbalimbali na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu na kwa upande wa umwagiliaji ulianza mwezi Juni mwaka huu na uanatarajiwa kukamilika mwezi April 2020

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com