METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, November 7, 2019

KATIBU MKUU TAMISEMI AAGIZA HALMASHAURI KUTOA ELIMU YA UJASIRIAMALI KWA WATU WENYE ULEMAVU


Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga,akizungumza  katika kongamano la majadiliano Wiki ya  asasi za kiraia (Azaki) linaloendelea jijini Dodoma 
Katibu Mkuu wa Shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata) Jonas Lubago,akiongea  wakati wa  kongamano la majadiliano Wiki ya  asasi za kiraia (Azaki) linaloendelea jijini Dodoma 

……………………

Na Alex Sonna

Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya watu wenye ulemavu ili wanufaike na mikopo inayotolewa na Halmashauri hizo.

Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga katika kongamano la asasi za kiraia (AZAKI) linaloendelea Jijini Dodoma.

Amesema watu wenye ulemavu wamekuwa hawatumii fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya ujasiriamali.

“Matokeo yake wanaishia kuishi maisha ya utegemezi na kuomba omba mitaani, ninajua kabisa watu wenye ulemavu hawawezi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha ikiwemo mabenki kutokana na hali yao, ndio maana serikali kwa kuliona hilo iliamua kutenga asilimia 2 kati ya 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi maalum yakiwemo ya watu wenye ulemavu,” amesema.

Ameeleza watu wengi wenye ulemavu bado hawajajitokeza vya kutosha kutumia fursa ya mikopo kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi hivyo wakurugenzi na maafisa hao wanatakiwa kutoa elimu ili waweze kujitokeza.

Amebainisha katika mwaka wa fedha 2018/19 Halmashauri nchini zilitenga jumla ya Sh. Bilioni 54.08  kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lakini mpaka kufikia Juni 30, mwaka huu kiasi cha fedha kilichokuwa kimetolewa ni Sh.Bilioni 42.06  ambapo vikundi vya watu wenye ulemavu walipata kiasi cha fedha Sh.Bilioni 3.87.

“Kwa mwaka wa fedha 2019/20 serikali imetenga kiasi cha fedha Sh.Bilioni 62.22 ambapo wanawake na vijana  wametengewa Sh.Bilioni 24.9 na watu wenye ulemavu wametengewa Sh.Bilioni 12.4,”amesema.

Naye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago amesema watu wengi wenye ulemavu hawana uelewa wa mikopo inayotolewa na Halmashauri nchini na ndiyo maana hawajitokezi kukopa.

Ameomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwakopesha watu wenye ulemavu wakiwa mtu mmoja mmoja maana wengi wanashindwa kutumia fursa ya mikopo kwa kukosa watu wa kujiunga nao kwenye vikundi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com